UBORESHAJI MATUMIZI YA LUGHA MAHAKAMANI KUTOA TUMAINI KWA WAARHIRIWA VITENDO VYA UKATILI

Hatua ya kuboresha matumizi ya lugha Mahakamani italeta matumaini mapya kwa waathirika wa vitendo vya ukatili, baada ya mahakimu, waendesha mashitaka na maafisa ustawi wa jamii kuanza kupewa mafunzo ya kutumia lugha yenye huruma na staha.

Mafunzo hayo yanawalenga wataalamu hao, ili kuwawezesha kuacha matumizi ya maneno yanayoweza kuongeza maumivu kwa waathirika wakati wa usikilizwaji wa kesi,na badala yake kuwa sehemu ya uponyaji na faraja kwa manusura wa ukatili.

Programu hiyo ya mafunzo inatolewa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, ikiwahusisha washiriki kutoka mikoa ya Mara na Simiyu, kwa lengo la kuwajengea ujuzi wa matumizi ya lugha rafiki, weledi na inayozingatia utu wa binadamu.

Akizungumza katika mafunzo hayo 13 Aprili 2026, Nabwike Ezekiah Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, amesema mabadiliko hayo yatasaidia kuimarisha utoaji wa haki bila kuathiri zaidi hisia za waathirika.

Baadhi ya washiriki akiwemo Chiza Kabwebwe na Eugenia Gerald wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi huku wakilinda heshima na utu wa wahanga.

Kwa upande wake mkazi wa mkoa wa Mara, Jacob Mnata amepongeza hatua hiyo akieleza kuwa italeta imani kwa wananchi katika mifumo ya haki.

Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Marlin Komba amesema ni muhimu kuhakikisha mazingira ya kimahakama yanakuwa salama kwa waathirika,ili waweze kutoa ushahidi bila hofu wala shinikizo.

Amesisitiza kuwa lugha inayotumika mahakamani ina nafasi kubwa katika kusaidia au kuumiza zaidi waathirika, hivyo ni lazima itumike kwa uangalifu mkubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *