UBINGWA MARA TANO: MASHABIKI WA YANGA KATAVI WAFANYA MATENDO YA HURUMA

Na Daniel Gahu – Katavi.

Mashabiki wa klabu ya Dar es Salaam Young Africans (Yanga) mkoani Katavi wameadhimisha kwa shangwe ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC pamoja na mafanikio ya timu hiyo dhidi ya watani wao wa jadi, Simba, katika michezo ya Dabi ya Kariakoo.

Sherehe hizo zimefanyika katika Ukumbi wa Idara ya Maji uliopo Manispaa ya Mpanda, zikihusisha burudani mbalimbali zilizoandaliwa na mashabiki hao ikiwa ni sehemu ya kusherehekea mafanikio ya timu yao.

Hata hivyo, tofauti na sherehe za kawaida za ushindi, mashabiki hao wameamua kuufanya ukumbusho huo kuwa wa kijamii zaidi kwa kushiriki katika shughuli za kuwasaidia wananchi wenye uhitaji.

Katika hatua hiyo, mashabiki hao wamefanya zoezi la kuchangia damu katika Benki ya Damu Salama iliyopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi.

Wakizungumza wakati wa zoezi hilo, mashabiki hao wamesema wameamua kuchangia damu kwa kutambua umuhimu wake katika kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu, huku wakisisitiza kuwa furaha ya mafanikio ya timu yao inapaswa kwenda sambamba na kugusa maisha ya jamii.

Mbali na uchangiaji damu, mashabiki hao pia wametembelea kituo cha kulelea watoto yatima kilichopo Kata ya Nsemulwa, ambapo wamekabidhi mahitaji mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya watoto wanaolelewa katika kituo hicho.

Akizungumza wakati wa kupokea misaada hiyo, mlezi wa kituo hicho amesema ujio wa mashabiki hao umeleta furaha na faraja kwa watoto, huku akiwapongeza kwa kuamua kutumia sehemu ya sherehe zao kuwakumbuka watoto wenye mahitaji maalumu.

Kwa upande wao, watoto wa kituo hicho wamewashukuru mashabiki hao kwa msaada waliowapatia, kabla ya kufanya ibada maalumu ya maombi kwa ajili ya kuwaombea mashabiki hao pamoja na timu yao.

Watoto hao wameiombea Yanga ifanye vizuri katika mashindano mbalimbali inayoshiriki, huku wakituma ujumbe kwamba mafanikio ya michezo yanaweza kuwa chachu ya kuleta upendo, mshikamano na msaada ndani ya jamii.

Kwa ujumla, sherehe hizo za mashabiki wa Yanga mkoani Katavi zimegeuka kuwa zaidi ya kushangilia mafanikio ya uwanjani, baada ya kuunganisha burudani, michezo, kuchangia damu na kutoa misaada kwa watoto wenye uhitaji — hatua inayodhihirisha namna furaha ya ushindi inavyoweza kutumika kuleta manufaa kwa jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *