TWAWEZA WAKABIDHI RASMI MRADI WA URAGHABISHI KWA SERIKALI

Na Tryphone Odace – Kigoma.

Shirika la TWAWEZA limekabidhi rasmi mradi wa uraghabishi kwa Serikali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, huku wadau wakieleza dhamira ya kuendeleza mafanikio yaliyopatikana baada ya mradi huo kukamilika.

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika leo Augost 28, 2026 katika Manispaa ya Kigoma Ujiji na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, wawakilishi wa TWAWEZA pamoja na waraghabishi walioshiriki katika utekelezaji wa mradi huo.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Jabiri Majira, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo alisisitiza umuhimu wa kuendeleza kazi zilizofanywa kupitia mradi huo ili kuhakikisha manufaa yake yanaendelea kuonekana katika jamii hata baada ya mradi kumalizika.

Kwa upande wake, mwakilishi wa TWAWEZA Bi. Ester Prosper ameeleza kuwa mradi huo umeleta mafanikio mbalimbali, ikiwemo kuwajengea uwezo waraghabishi na kuwawezesha kushiriki katika kuhamasisha jamii kuhusu masuala mbalimbali yenye umuhimu kwa maendeleo ya wananchi.

Amesema uzoefu na ujuzi walioupata waraghabishi kupitia mradi huo ni miongoni mwa rasilimali muhimu zitakazosaidia kuendeleza shughuli hizo kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine.

Baadhi ya waraghabishi walioshiriki katika mradi huo akiwamo Sofia Patrick walieleza kuwa wamepata uelewa na uwezo mkubwa wa kushirikisha jamii, kuibua changamoto zinazowakabili wananchi na kuhamasisha hatua za kuzitatua.

Wameeleza kuwa baada ya mradi kuisha, wataendelea kutumia ujuzi na uzoefu walioupata kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali na wananchi katika kuhakikisha shughuli za uraghabishi zinaendelea kuwa na matokeo chanya.

“Tunaahidi kuendeleza ushirikiano na kutumia fursa zilizopo katika jamii ili kuhakikisha mafanikio ya mradi huo hayapotei, bali yanaendelea kuleta matokeo kwa wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji ikiwemo kukomesha ukatili” alisema Patrick.

Aidha makabidhiano hayo yameonekana kuwa hatua muhimu ya kuhakikisha shughuli zilizotekelezwa kupitia mradi huo zinaendelezwa na kuwa sehemu ya juhudi endelevu za jamii katika kushughulikia changamoto na kuchochea maendeleo.

Kwa upande wake, Naibu Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Mgeni Kakolwa amesema kupitia mradi wa uraghabishi miradi mbalimbali iliyoibiliwa na wananchi imekamilika ikiwem zahanati, barabara na upimaji wa ardhi zilikuwa hazijapimwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *