Na Gideon Gregory – Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka amesema Wizara hiyo itafanya utafiti wa uanzishwaji wa Benki ya Vijana wenye lengo la kuchambua kwa kina ili kuwa na taasisi maalum ya kifedha itakayojikita katika mahitaji ya vijana.
Waziri Nanauka ameyasema hayo leo Aprili 20, 2026 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
“Dhamira ya Serikali ni kuweka msingi wa mfumo wa kifedha unaoendana na mazingira na uwezo wa vijana wengi, hususani wale wanaoanza shughuli za kiuchumi, ili kuondoa vikwazo vilivyopo katika upatikanaji wa mitaji,” amesema.

Amesema Benki ya Vijana, itakayoanzishwa, itakuwa chombo muhimu cha kimkakati kitakachowezesha upatikanaji wa huduma za kifedha zilizo rafiki kwa vijana, kuchochea ubunifu wa bidhaa za kifedha zinazolingana na mahitaji yao, kupanua wigo wa uwekezaji wa vijana, na hatimaye kuongeza ajira na mchango wa vijana katika kukuza uchumi shindani na jumuishi wa Taifa.
Aidha, Nanauka amesema katika kuimarisha ukuzaji wa biashara na uwezeshaji wa vijana kiuchumi, Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya kujenga uwezo kuhusu ujasiriamali na ujuzi wa usimamizi wa biashara kwa vikundi vya vijana nchini ikiwemo kutoa mikopo nafuu kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili waweze kujiajiri ka kuajiri wengine.
“Aidha, Serikali itafanya utafiti wa uanzishwaji wa vituo vya ubunifu vya kitaifa kwa vijana pamoja na kuanzisha vituo vya ubunifu kwa vijana (VIJANA Hub) vitakavyolenga kukuza ubunifu, kuendeleza vipaji, kutoa huduma za uratibu wa mawazo ya biashara,”
“Pamoja na kuwaunganisha vijana na fursa za masoko, teknolojia na mitaji kwa ajili ya kuongeza ushindani na tija katika shughuli zao za kiuchumi; kuandaa Mwongozo wa Kitaifa wa fursa za uwezeshaji kiuchumi ndani na nje ya nchi,” amesema.
Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, zinaonesha kuwa Tanzania Bara ina jumla ya vijana 20,612,566 wenye umri wa miaka 15 hadi 35 ambao ni sawa na asilimia 34.4 ya idadi ya watu wote, Aidha, kwa mujibu wa Utafiti wa Nguvu Kazi wa Mwaka 2020/21, vijana wanachangia zaidi ya asilimia 55 ya nguvu kazi ya Taifa.
Katika Mwaka 2026/27, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana imeliomba Bunge liidhinishe kiasi cha jumla ya Shilingi Bilioni 35.


