Rais Paul Kagame amesema Rwanda haiwezi kukaa kimya wakati usalama wake unahatarishwa na Nchi ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) huku akidai kuwa wamejaribu mara nyingi kuzungumza na Kongo bila mafanikio.
Rais Kagame ameyasema hayo hii leo Februari 8, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha Wakuu wa SADC na EAC huku akisisitiza kuwa suluhisho la kudumu kuhusu mzozo huo linahitajika na si kuelekeza lawama kwa Rwanda kwa matatizo yanayotokea DRC.

Amesema, “hawawezi kutuambia tukae kimya wakati wanasababisha matatizo makubwa ya kiusalama dhidi yetu, hakuna wa kutuambia tukae kimya, tumeongea na Kongo mara nyingi tumewaita tukae tuongee hawataki.”
“Mimi naomba tusiwe na vikao vingi sana. Hatuwezi kila siku kukaa kujadili matatizo maana kinachoendelea pale ni vita ya Kikabila ni suala la kutambuana, kujadiliana na kuwapa haki yao, tutumie kikao hiki kupata suluhu ya kudumu,” amesema Kagame.