TUSIWATENGE WALA KUWANYANYAPAA WENYE ULEMAVU – RC MTANDA

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ametoa wito kwa jamii kuwajali watoto wenye tatizo la Down Syndrome na kuhakikisha wanawapatia huduma za kijamii kama elimu na afya na kuacha tabia ya kuwatenga na kuwanyanyapaa.

Mtanda ametoa wito huo Machi 21, 2025 wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Down Syndrome ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya furahisha jijini Mwanza.

Mtanda amesema katika kuwathamini watoto wenye tatizo hilo jamii inatakiwa kuwajali na kuhakikisha wanapata huduma zote za kijamii kama vile huduma za afya, elimu huku pia jamii ikiacha utaratibu wa kuwanyanyapaaa.

“Watu wenye ulemavu wana uwezo wa kufanya mambo makubwa sana, tusiwafiche watoto wenye tatizo hili wala ulemavu wa aina yoyote, na tuwakumbushe kuwa watakaowalea vizuri wenye tatizo hili basi mbele ya Mwenyezi Mungu wana daraja na fungu lao la thawabu,” Mtanda amefafanua.

Katika hatua nyingine Mtanda pia ametoa wito kwa watoa huduma za kijamii hususani wahudumu wa  sekta ya afya kuhakikisha wanafuatilia utekelezaji wa matamko ya Serikali na namna ya kutekeleza katika kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa kundi hilo kwa mujibu wa sera ya afya inavyotambua kisheria.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amewataka wanawake wajawazito kua na desturi ya kufanya uchunguzi na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya kwani endapo watafuata ushauri huo watato watakaozaliwa wataweza kukua vizuri kiafya.

 Naye, Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Down Syndrome nchini Mony Teri Pettit ameiomba serikali kuhakikisha inaweka mifumo mizuri ya kutoa huduma za afya huku ikiendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya ugonjwa huo ili watoto watoto hao waweze kudhaminiwa.

Siku ya Kimataifa ya Down Syndromes ambayo kitaifa imefanyika Mwanza imeongozwa na kaulimbiu isemayo ”Mifumo ya Huduma za Kutuwezesha Iboreshwe.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *