TUMIENI FURSA MIKOPO YA ASILIMIA 10 KWA UWEKEZAJI, KUBADILI MAISHA – MEYA MAULID

Na Tryphone Odace – Kigoma.

Wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, wametakiwa kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 10, inayotolewa na Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri, kwa kuwekeza katika shughuli za kiuchumi zitakazowawezesha kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.

Wito huo ulitolewa hii leo Augost 28, 2026 na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mussa Maulid, wakati wa hafla ya mafunzo kuhusu namna ya kutumia mikopo ya asilimia 10 pamoja na kukabidhi mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mussa alisema mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kiuchumi na kwamba fursa hiyo haikulenga wanawake pekee, bali makundi yote yaliyowekwa katika utaratibu wa kunufaika na mikopo hiyo.

“Ni muhimu wananchi wenye sifa kuchangamkia mikopo hii na kuitumia katika shughuli zenye tija ili iweze kutimiza lengo la Serikali la kuwawezesha wananchi kiuchumi” alisema Mussa.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Jabiri Majira Msumi, alisema katika mwaka 2025 jumla ya vikundi 109 vilinufaika na mikopo hiyo.

Msumi alisema Manispaa hiyo imejipanga kuongeza wigo wa wanufaika katika mwaka 2026 kwa kuhakikisha makundi mengi zaidi yanapata fursa ya mikopo hiyo na kutumia fedha hizo kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Aliongeza kuwa mafunzo yanayotolewa kwa wanavikundi ni sehemu muhimu ya kuwawezesha wanufaika kuelewa matumizi sahihi ya fedha za mikopo na namna ya kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.

Baadhi ya wanavikundi walionufaika na mikopo hiyo wameeleza kuwa mafunzo waliyopatiwa yatawasaidia kuwa na uelewa zaidi kuhusu matumizi sahihi ya fedha na namna ya kuimarisha biashara zao.

Wamesema elimu hiyo itawasaidia kufanya maamuzi sahihi katika matumizi ya mikopo, kuongeza tija katika shughuli zao na hatimaye kukuza mitaji na biashara zao.

Serikali inaendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri kwa makundi mbalimbali, ikiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi na kuongeza uwezo wa kujiajiri, huku wanufaika wakisisitizwa kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhakikisha mikopo hiyo inaleta matokeo chanya kwao na kwa jamii kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *