Tume ya mazungumzo ya kitaifa nchini Senegal imependekeza uchaguzi mkuu wa urais kufanyika tarehe 2 ya mwezi Juni mwaka huu hatua inayokuja baada ya tarehe ya awali kucheleweshwa.
Afisa wa tume hiyo Ndiawar Paye, ameeleza kuwa licha ya mapendekezo hayo rais Macky Sall, atasalia ofisini hadi pale ambapo mrithi wake atakapochaguliwa na kuapishwa.
Taifa hilo la Afrika Magharibi limekuwa linakabiliwa na mzozo wa kisiasa tangu rais Sall atangaze kuhairishwa kwa tarehe ya uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 25 ya mwezi huu wa Februari.
Tume hiyo imeafikia mapendekezo hayo baada ya kufanyika kwa mazungumzo ya siku mbili yalioratibiwa na rais Sall kama njia moja ya kupunguza joto la kisiasa ambalo limeshuhudiwa.
Kwa sasa mapendekezo hayo yanatarajiwa kutumwa kwa mkuu wa nchi ambaye atafanya maamuzi ya mwisho ila haijabainika iwapo rais atapinga au kuridhia.
Mazungumzo yaliofanyika jijini Dakari yalisusiwa na baadhi ya wanasiasa wa upizani wanasisitiza ni lazima uchaguzi huo ufanyike kabla ya muda wa rais Sall kuhudumu kumalizika tarehe mbili ya mwezi ujao.
Licha ya mapendekezo hayo, haijulikani iwapo pia upinzani utaridhia mapendekezo ya tume.