Na Saada Almasi, Bariadi – Simiyu.
Katika kuendelea kujenga mahusiano mazuri kati ya jamii, Jeshi la Polisi Mkoani Simiyu likiongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP. Edith Swebe limeongoza jopo la Madaktari kutoka Zahanati ya polisi kupima afya waamini wa dini ya Kiislamu, waliokuwa wakishiriki ibada katika Msikiti Mkuu wa BAKWATA Mkoa wa Simiyu, uliopo mjini Bariadi.
Katika zoezi hilo Kamanda Swebe amewataka waamini kuwa na desturi ya kuangalia afya zao mara kwa mara, ili kuendelea kujiweka sawa na kuepuka madhara ya ghafla ambayo yanaweza kujitokeza, pasi na mtu kuwa na uelewa wa kile ambacho angeweza kuepukana nacho kwa kupata matibabu tangu awali.

“Wengi wetu tunatembea tukiwa hatujui kama tunaumwa ,kwa hiyo mtu ukipata tu changamoto ya ghafla ni rahisi kuathirika zaidi lakini tukiwa na utaratibu wa kujua afya zetu ni rahisi kuanza matibabu mapema na kujiweka salama zaidi,” amesema Kamanda Swebe
Katika hatua nyingine Jeshi hilo limechangia damu katika benki ya damu hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu ,kufanya usafi wa mazingira ya hospitali hiyo pamoja na kutoa zawadi mbali mbali kwa wagonjwa wanaoendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

Akipokea zawadi hizo Mratibu wa Huduma za Tiba hospitalini hapo Dokta Juma Muna amelipongeza jeshi hilo kwa kujitoa kwao kuona walio na mahitaji na kuwasaidia huku akitoa wito kwa wananchi zaidi kuendelea kushiriki katika matendo mbalimbali yanayoihusisha jamii ili kudumisha upendo miongoni mwao.
“Kwa niaba ya wagonjwa ambao wanafikishiwa zawadi hizi siku ya leo niwashukuru sana Jreshi la Polisi hiki mlichofanywa ni kitu kikubwa na cha kuigwa katika jamii,mmetusaidia damu katika benki yetu ambayo inakwenda kuokoa maisha ya wengu na niwaombe jamii yote tuendelee kuwa na moyo wa kujitolea kwani ni wengi walio na mahitaji lakini wanakosa watu wa kuwasaidia,” amesema Dokta Muna.



