Na Saulo Stephen – Singida.
Mgombea Udiwani katika Kata ya Mitunduruni Jimbo la Singida Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Valerian Kimambo amewataka wananchi wa kata hiyo kuichagua CCM kuanzia nafasi ya Udiwani, Ubunge pamoja na Urais, ifikapo Oktoba 29, Mwaka huu.
Kimambo ameyazungumza hayo wakati akinadi sera kwa Wananchi wa Kata ya Mitunduruni kwenye mkutano wa kampeni za CCM, uliofanyika viwanja Msufini Kata ya Mitunduruni Mjini Singida.
Amesema, licha ya yeye kuwa Mgombea pekee wa Udiwani katika Kata hiyo, haimaanishi kuwa tayari amepita, kwani wana CCM na wana Mitunduruni wanapaswa kujitokeza kupiga kura za ndio kwa wingi, ili aendelee kuleta maendeleo kwa Wananchi wa Kata ya Mitunduruni.

Akimuombea kura Mgombea Ubunge wa jimbo la Singida Mjini, Yagi Maulid Kiaratu Kimambo amesema anamfahamu vizuri yagi kwani amefanya nae kazi kwa kipindi cha mika 10 akiwa Kaimu mstahiki meya kwa miaka 5 na Mstahiki meya wa Manispaa ya Singida kwa miaka mingine mitano.
Amesema, anaamini anatosha kuwa Mbunge wa jimbo la Singida Mjini, kutokana na uzoefu wake katika uongozi ikiwemo usimamizi mzuri wa Miradi ya maendeleo, huku akiwaomba wanamitunduruni kumpigia kura Mgombea urais wa chama hicho Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi wa Oktoba 29.


