TUHUMA ZAIBUKA MTOTO ALIYEUAWA NA FISI ITILIMA

Na Saada Almasi – Simiyu.

Hofu imetanda kwa wakazi wa Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu hususan waishio maeneo ya Vijijini, kutokana na uwepo kwa Wanyama wakali wakiwemo fisi ambao wamesabaisha mauaji mauaji kwa nyakati tofauti huku baadhi ya Watu wakidai Fisi hao wanaagizwa na watu.

Hali hiyo, imesabishwa na tukio la hivi karibuni la mauaji ya mtoto Saenda Kusendeka (3), wa kijiji cha Mhunze kilichopo Wilayani humo kushambuliwa na kuuawa na fisi akiwa na mama yake nyumbani kwao na kufanya jumla ya watu wanane kufariki kwa kushambuliwa na Wanyama hao ndani ya miezi mitatu mfululizo.

Baba mzazi wa mtoto huyo, Kusendeka Saenda amesema mtoto wake alienda kukaa na mama yake na wakati wakiandaa chakula cha jioni ndipo fisi huyo aliwavamia na kusabababisha kifo cha mwanae.

“Huyu mtoto alikuwa na mama yake anachambua mboga walikuwa wanaandaa chakula cha jioni alipenda kuwa na mama yake mimi sikuwepo lakini nilipigiwa simu kuna tukio nyumbani nilipofika hapa tayari tukio limetokea na watu wanakimbia kumtafuta fisi ,ukweli nilishindwa niliishiwa nguvu,” alisimulia Kusendeka.

Awali, wakazi wa Kijiji hicho walidai kusikikitishwa na kitendo hicho, huku wakitaja matukio hayo kutokea kwa Imani za kishirikina wakiamini kuwa fisi hao hawakuwa Wanyama bali ni watu huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Edith Swebe akiahidi kufuatilia suala hilo.

Amesema, “matukio haya yamezidi sasa yalianzia wilaya ya Busega tukapambana yakaisha sasa ni Itilima kama ni kweli hawa siyo fisi basi ni vema na sisi tupite katika njia hizo ili tuweze kuwabaini wanaohusika maana mtaendelea hivi hadi lini?.”

Naye Mtemi wa Sungusungu Kijijini hapo, Mashini Malugu ameiomba Serikali kuwaruhusu kuwaua Wanyama hao, kwani pale wanapowajaribu kukabiliana nao Askari wa Wanyamapori huingilia kati na kuwakamata.

“Tunaomba Serikali iwaachie sungusungu wafanye kazi maana kila tunapowaua hawa fisi wanapokuja Askari wa Wanyamapori wanatukamata sasa na sisi tunaogopa,“ alisema mzee Malugu.

Kwa upande wake msimamizi wa Wanyamapori toka pori la akiba Maswa, Lawrence Okode amesema hadi sasa wameshafanikiwa kuwaua fisi tisa ambao kati yao wawili waliuawa na Wananchi, huku akiahidi kuendelea kushirikiana na jamii hiyo katika kuwadhibiti Wanyama hao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *