Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Erasto Makala amewataka Wakazi wa Wilaya ya Kibaha kuendelea kudumisha Upendo, amani na uimarishaji wa shughuli za kiuchumi huku akiwakaribisha watu kuwekeza katika eneo hilo.
Makala ameyabainisha hayo wakati akizungumza na Wanahabari Ofisini kwake mjini Mlandizi, Kibaha Pwani juu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika Wilaya hiyo, ambayo amesema inayoendelea kukua kwa kasi.

Amesema, “Mwaka 2022/2023 tulishakuwa wa kwanza kitaifa kwa kuongoza kimapato na kila mwaka kuna ongezeko sasa hivi tumeenda hadi asilimia 200 mpaka 300 lakini kikubwa Kibaha tunajivunia zaidi upendo, ukarimu, watu wake ni wacheshi na sehemu yenye ucheshi kuna upendo.”

Aidha, Makala pia aliagiza maafisa maendeleo ya jamii kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa elimu, akibainisha kuwa baadhi ya wanafunzi wenye uwezo wa kufaulu wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na shinikizo la wazazi wao, ambao wanawashinikiza kufeli, ili waolewe au kuchunga mifugo.
Sambamba na hatua hiyo, Makala aliwataka pia Maafisa elimu kuandaa siku maalum ya wadau wa elimu kwa ajili ya kujadili changamoto zinazokwamisha maendeleo ya sekta hiyo na kutafuta suluhisho la pamoja.