Na Pascal Tuliano – Tabora.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Dkt. John Pima ametoa wito kwa Waendesha Bodaboda, Mama lishe pamoja na wamiliki wa magari yanayobeba abiria, kuhakikisha wanadumisha usafi katika maeneo yao ya kazi.
Akizungumza leo katika Stendi ya zamani katikati ya mji wa Tabora mara baada ya kuzindua Wiki ya Usafishaji Duniani kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, Dkt. Pima amesema suala la usafi ni jukumu la kila mmoja.

Amesema, maeneo ya bodaboda yatakayobainika kuwa machafu yatafungwa mara moja, huku wamiliki wa magari ya abiria wasio na vyombo vya kuhifadhia taka wakikabiliwa na faini kwa mujibu wa sheria za Manispaa na za Taifa.
“Tabora tuna nafasi kubwa ya kuwa Jiji, lakini hatuwezi kufanikisha ndoto hiyo ikiwa mji wetu utabaki mchafu. Sifa kuu ya Jiji ni kuwa na mazingira safi kila wakati,” amesema Dkt. Pima.

Aidha, ameagiza watendaji wa mitaa, viongozi wa kata pamoja na maafisa afya kuhakikisha wanalisimamia ipasavyo zoezi la usafi kwa kila kaya na taasisi ili kudumisha mji wenye mandhari ya kupendeza.
Kwa mujibu wa Dkt. Pima, yeyote atakayekaidi maagizo ya kufanya usafi atachukuliwa hatua kali za kisheria bila upendeleo.


