TRA YATOA ELIMU MABADILIKO SHERIA MPYA ZA KODI KWA WAFANYABIASHARA KAGERA

Na Cecilia Shiratu, Bukoba – Kagera.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kagera imeanza kutoa Semina ya mabadiliko ya sheria mpya 17 za kodi kwa wafanyabiashara Mkoani humo zilizopitishwa na bunge kwa mwaka wa fedha  2026/2027  kwa lengo kuongeza wigo wa ulipaji kodi na kuwaepusha faini na adhabu amabazo ziaweza kuathiri mfumo wa ulipaji kodi.

Kaimu Meneja wa Mamlaka ya hiyo Mkoa wa Kagera, Estomih Mossi, amesema mabadiliko ya sheria hizo yanalenga urasimishaji wa biashara na kutoa msamaha wa kodi kwa anayeanza biashara na kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) na atapewa msamaha kwa kipindi cha miezi 12 kufanya biashara zake bila malipo yoyote.

Aidha, amesema TRA imeendelea kuimarisha mifumo ya ulipaji kodi kwa njia za kielektroniki, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kurasimisha biashara na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

Kwa upande wake, Meneja wa Chama cha Wafanyabiashara Mkoa wa Kagera, Rwechungula Mali, amesema utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara ni muhimu kwa sababu ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu sheria za kodi unaweza kusababisha changamoto katika utekelezaji wa shughuli zao.

Mali ameiomba TRA kuendelea kuyafanyia kazi maoni na changamoto zilizowasilishwa na wafanyabiashara na kusisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mfumo wa kodi rafiki unaomwezesha mfanyabiashara kufanya biashara, kupata faida na hatimaye kuwa na uwezo wa kutimiza wajibu wake wa kulipa kodi.Mazingira mazuri ya biashara yanaweza pia kuvutia wafanyabiashara kutoka nchi jirani, ikiwemo Uganda, kuja kufanya biashara nchini.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Kagera, Nicolaus Jovin, amesema bajeti ya mwaka huu imelenga kukuza uchumi kwa kuweka mazingira ya kimkakati yatakayoiwezesha Kagera kutumia nafasi yake ya  kuwa lango la biashara kutokana na kupakana na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi.

Jovin ameongeza kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele ni kurasimisha wafanyabiashara walio katika sekta isiyo rasmi, kuboresha mifumo ya kodi, kurahisisha ulipaji kodi katika maeneo ya mipakani, kuweka utaratibu wa misamaha ya kodi kwa maeneo yanayostahili pamoja na kulinda bidhaa za ndani dhidi ya biashara za magendo.

Kwa upande wao,wafanyabiashara katika manispaa ya Bukoba  wameeleza kuwa licha ya baadhi ya mabadiliko kuwa na manufaa, bado kuna maeneo wanayoona yanawaweka katika mazingira magumu, hususan wajasiriamali wenye mitaji midogo ambao hawakunufaika kwa kiwango kinachotarajiwa na misamaha ya kodi iliyotolewa katika baadhi ya sekta kama madini na utalii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *