Na Clavery Christian – Kagera.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya ziara maalum katika Mkoa wa Kagera kwa lengo la kuwatembelea Wafanyabiashara na walipa kodi wazuri, kusikiliza changamoto zao na kuwapongeza kwa uzalendo wao katika kuchangia mapato ya taifa kupitia ulipaji mzuri wa kodi.
Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuhitimisha mwaka wa fedha na kujiandaa na mwaka mpya wa fedha 2025/2026, ambapo kaimu mkurugenzi wa ununuzi kutoka TRA Makao Makuu, Ramadhani Mgarula akiwa na Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera na maafisa wengine wa TRA wametembelea maeneo mbalimbali ya biashara, kuzungumza na wafanyabiashara na kutoa elimu kuhusu kodi.
Akizungumza katika ziara hiyo, kaimu mkurugenzi wa ununuzi kutoka TRA Makao makuu Ramadhani Mgarula alisema kuwa lengo kuu ni kujenga mahusiano bora na walipa kodi, kusikiliza kero zao kwa ukaribu, na kuhakikisha wanapatiwa majibu kwa wakati ili kurahisisha mazingira ya kufanya biashara nchini.

“Tunathamini mchango wa wafanyabiashara hawa kwa uchumi wa Taifa. Tumekuja kuwasikiliza, kuwapongeza, lakini pia kuhakikisha kero zao zinatatuliwa kwa wakati,” alisema Mgarula.
Nao baadhi ya wafanyabiashara waliotembelewa walitumia fursa hiyo kuwasilisha changamoto mbalimbali, zikiwemo ucheleweshaji wa baadhi ya huduma, uelewa mdogo wa baadhi ya mifumo ya ulipaji kodi, na umuhimu wa elimu ya mara kwa mara kuhusu mabadiliko ya sheria za kodi.

Hata hivyo, walimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kwa kusisitiza kuwa serikali iendelee kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyabiashara, hali iliyowafanya wajisikie kuthaminiwa.
TRA imeahidi kuendeleza mashirikiano hayo na kuwatambua walipa kodi bora kila mwaka kama njia ya kuhamasisha ulipaji sahihi wa kodi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.