TRA TENGENEZENI URAFIKI NA WAFANYABIASHARA KURAHISISHA UKUSANYAJI WA MAPATO – RAIS SAMIA

Na Saada Almasi – Simiyu.

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka watumishi wa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kutengeneza urafiki na Wafanyabiashara, ili waweze kurahisisha ukusanyaji wa mapato ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo hutumika katika kuleta maendeleo ya nchi.

Amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na watumishi hao muda mchache baada ya kuzindua jingo la mamlaka hiyo lililopo kata ya Somanda wilayani Bariadi mkoani Simiyu na kusema kuwa maendeleo yanayofanywa na serikali yanatokana na mapato ya ndani kwa kiasi kikubwa hivyo wanatakiwa kukaa meza moja na kuwafanyabiashara ili waone namna ya kulipa kodi bila kikwazo.

“kati ya miradi yote sita ninayoizindua leo ni mradi mmoja tu ambao ni binafsi iliyobaki ni miradi ya serikali ambayo imetokana na mapato ya ndani ,sasa niwaombe tukae vizuri na wafanyabiashara vizuri tuwasikilize tukubaliane ni namna gani watalipa madeni yao taratibu bila kuwaumiza maana kidogo kidogo atamaliza deni lote tu japokuwa wapo wadaiwa sugu nao mtafute namna ya kuwaingia,” amesema Raisi Samia.

Sambamba na hilo Rais Samia amesema kuwa kwa sasa serikali imeongeza ajira kwa watumishi wa mamlaka hiyo hadi kufikia 1800 ili kutia nguvu katika utendaji kazi huku akiwataka kuweka kipaumbele katika kuwapa elimu walipa kodi ili waone faida ya kulipa kodi.

“nimeagiza nguvu iongezwe katika mamlaka hii na sasa watumishi wengine 1800 wataongezwa lengo ni kuongeza nguvu katika utendaji kazi lakini bado kuna wafanyabiashara wanatembelewa na maafisa hawajui chochote kuhusu kodi hebu msitumie nguvu mkaweka uadui bali waelimisheni waone faida ya kulipa kodi,” ameongeza Rais Samia.

Naye Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema kuwa mkoa wa Simiyu hadi sasa umevuka kusudi la kukusanyo lililokuwa la shilingi Bilioni 22 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na kukusanya shilingi Bilioni 25 ,makusanyo yaliyochangiwa na kuwepo kwa vitendea kazi bora katika mkoa huo.

“Kwepo kwa hili jengo na vitendea kazi bora kumetoa hamasa kubwa katika ukusanyaji wa mapato hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha tulikuwa na makadirio ya kukusanya shilingi Bilioni 22 lakini tumevuka lengo na kufikia kiasi cha shilingi bilioni 25 hayo ni mafanikio makubwa kwetu,” amesema Yusuph.

Rais Samia Suluhu yupo katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu ambapo wilayani Bariadi amezindua kiwanda cha Nondo NGS ,jingo la TRA,ofisi ya mkuu wa mkoa huo, ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Shule ya Sekondari ya Wasichana Simiyu pamoja na kuzindua Chanjo ya Mifugo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *