Katika kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema itaweka kumbukumbu za kikodi katika makumbusho ya Mwalimu, wilayani Butiama mkoani Mara, hatua inayolenga kuenzi misingi aliyoiamini kuhusu uwazi, uwajibikaji na umuhimu wa kodi katika ujenzi wa Taifa.
Akizungumza mara baada ya kutembelea kijiji cha Mwitongo, nyumbani kwa Baba wa Taifa, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda,amesema mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha falsafa ya Mwalimu kuhusu kujitegemea na ushiriki wa wananchi katika ulipaji wa kodi inaendelea kuenziwa na kutekelezwa kwa vitendo.

Mwenda amesema TRA itaendelea kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari miongoni mwa Watanzania, akibainisha kuwa mchango huo ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya Taifa na kuboresha huduma za kijamii.
Aidha, amesisitiza kuwa uwekaji wa kumbukumbu za kikodi katika makumbusho ya Mwalimu utasaidia vizazi vya sasa na vijavyo kuelewa kwa kina mchango wake katika kujenga msingi wa uwajibikaji na uwazi, pamoja na kuhamasisha uzalendo katika suala la kodi.

Katika hatua nyingine, Mwenda amesema mamlaka hiyo itaendelea kuhakikisha inatekeleza kwa vitendo maono ya Mwalimu kwa kuweka mifumo rafiki ya ulipaji kodi na kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchangia maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, mtoto wa Baba wa Taifa Madaraka Nyerere amepongeza hatua hiyo, akisema inaonesha namna Watanzania wanavyoendelea kumuenzi na kuthamini mchango wa Mwalimu katika kujenga Taifa lenye misingi imara ya uwajibikaji, uwazi na uzalendo.


