TPF NET KATAVI YAONGEZA UAFANISI UTOAJI HUDUMA BORA KWA JAMII

Na Daniel Gahu – Katavi.

Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Polisi Tanzania (TPF NET) Mkoa wa Katavi umeendelea kuimarisha umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa askari wanawake, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi na kuboresha huduma kwa jamii.

Hatua hiyo imejidhihirisha Septemba 01, 2026, wakati wa kikao cha utendaji kazi cha TPF NET Mkoa wa Katavi kilichoongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Kaster Ngonyani, kilichofanyika katika Ukumbi Mdogo wa Polisi Kantini.

Akizungumza katika kikao hicho, Kamanda Ngonyani amesisitiza umuhimu wa kuwa na umoja na mshikamano miongoni mwa askari wanawake, akieleza kuwa misingi hiyo ni nguzo muhimu katika kufanikisha majukumu ya TPF NET pamoja na yale ya Jeshi la Polisi kwa ujumla.

Amesema kuwa askari wanawake wana nafasi kubwa katika kujenga taswira nzuri ya Jeshi la Polisi kupitia namna wanavyowahudumia wananchi, hivyo ni muhimu kuhakikisha kila mmoja anatekeleza majukumu yake kwa weledi, uadilifu na kuzingatia misingi ya maadili ya Jeshi hilo.

Kamanda Ngonyani amewataka askari wanawake hao kuwa mfano katika jamii kwa kutoa huduma zenye heshima, upendo na utu, akisisitiza kuwa namna askari anavyowasiliana na mwananchi ni sehemu muhimu ya kujenga imani na ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.

Aidha, ameeleza kuwa ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wanachama wa TPF NET unapaswa kwenda sambamba na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu, ili mtandao huo uweze kutimiza malengo yake na kutoa mchango chanya katika jamii.

Kikao hicho pia kimekuwa sehemu ya kuwakumbusha askari wanawake umuhimu wa kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kuimarishana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Kwa msisitizo huo, TPF NET Katavi imeendelea kuweka mbele ajenda ya umoja, mshikamano na huduma bora kwa wananchi, huku ikilenga kuhakikisha askari wanawake wanakuwa chachu ya mabadiliko, nidhamu na ufanisi ndani ya Jeshi la Polisi na katika jamii kwa ujumla.

y

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *