Na Gideon Gregory – Dodoma.
Kwa miaka mingi wakulima wa ndizi nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutumia miche isiyoidhinishwa jambo lililochangia kuenea kwa magonjwa, kushuka kwa uzalishaji na kupungua kwa kipato.
Hata hivyo, matumaini mapya yameanza kuonekana baada ya Serikali kusajili aina 12 za ndizi zitakazoweka msingi wa upatikanaji wa miche bora na salama kwa wakulima.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Agosti 7,2026 Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya kudhibiti ubora wa mbegu Tanzania (TOSCI), amesema usajili wa aina hizo za ndizi ni hatua muhimu katika kuhakikisha wakulima wanapata miche iliyothibitishwa, yenye uwezo wa kuongeza tija na kustahimili changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Kwa muda mrefu Tanzania haikuwa na miche ya ndizi iliyosajiliwa rasmi, hali iliyowafanya baadhi ya wakulima kubadilishana miche bila uhakika wa ubora wake kupitia usajili huo, sasa kutakuwa na chanzo rasmi cha kuzalisha na kusambaza miche bora kwa wakulima,” amesema.
Aidha, amesema Serikali kupitia TOSCI inaendelea kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) pamoja na sekta binafsi ili kuongeza uzalishaji wa miche bora ya ndizi na kuhakikisha inawafikia wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa TOSCI, Kituo cha Utafiti cha Maruku kilichopo mkoani Kagera kimepewa jukumu la kuendelea kufanya tafiti na kubaini aina mpya za ndizi zinazoweza kuongeza uzalishaji na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika kilimo hususani matika mkoa huo.
Mbali na hatua hiyo, TOSCI imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya biashara ya mbegu feki kwa kufanya ukaguzi wa maduka ya pembejeo, kutoa elimu kwa umma na kuwafikisha wahusika wanaokiuka sheria kwenye vyombo vya sheria.
“Niwaombe wakulima kuhakikisha wananunua mbegu na miche yenye lebo ya uthibitisho wa TOSCI, kudai risiti kila wanapofanya ununuzi na kutumia huduma za uthibitishaji ili kujiridhisha na ubora wa mbegu kabla ya kuzipanda,”amesema.
Hatua hizo zinaonesha dhamira ya Serikali ya kujenga sekta ya mbegu yenye ubora, kuongeza uzalishaji wa mazao ya kimkakati kama ndizi na kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo bora zitakazoongeza kipato kuimarisha usalama wa chakula na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kilimo.


