TMDA YAWEKA MKAKATI KUKABILI WIMBI LA DAWA BANDIA KANDA YA ZIWA

Na Adam Msafiri – Mara.

Wimbi la dawa bandia limechukua sura mpya katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, jambo linalohatarisha afya za binadamu na mifugo, ambapo Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imechukua hatua za haraka kukabiliana na mbinu hizo mpya.

Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa, Agrey Mwabuki amesema mamlaka hiyo imeanza kutoa mafunzo kwa watendaji wake waliopo katika halmashauri za mkoa wa Mara ili kuwajengea uwezo wa kudhibiti matumizi na usambazaji usio sahihi wa dawa na vifaa tiba.

“Tunawafanyia mafunzo watendaji wetu kuwajengea uwezo, weledi na mbinu mbalimbali za kikaguzi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Lengo ni kulinda afya ya jamii kwa kuhakikisha bidhaa zinazozunguka katika maeneo yao ni salama, bora na zenye ufanisi,” amesema Mwabuki.

Kwa upande wake Venancy Burushi, Mkaguzi Mwandamizi kutoka TMDA Kanda ya Ziwa ameitaka jamii kujenga tabia ya kusoma na kujiridhisha taarifa zilizopo kwenye vifungashio vya dawa kabla ya matumizi,ili kuepuka kutumia dawa zilizopitwa na wakati au bandia ambazo zinaweza kusababisha madhara makubwa kiafya.

Nao baadhi ya watendaji wa TMDA wanaoshiriki mafunzo hayo wamesema yataongeza uelewa na kuimarisha vita dhidi ya uuzaji wa dawa bandia,unaoendelea kushamiri katika maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *