Matumizi yasiyo sahihi ya dawa za mifugo yameendelea kuwa changamoto katika sekta ya ufugaji, huku baadhi ya wafanyabiashara wakitajwa kuuza dawa hizo bila kuwa na utaalamu, hali inayochangia ongezeko la usugu wa vimelea vya magonjwa.
Hayo yamebainishwa na Mshauri wa Mifugo Mkoa wa Mara, Mathias Lusheleja,wakati wa mafunzo ya uhamasishaji kwa wafugaji kuhusu mapambano dhidi ya usugu wa vimelea kwa dawa, yaliyofanyika katika Manispaa ya Musoma.

Amesema, kuna haja ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuongeza nguvu katika kudhibiti utoaji wa leseni za maduka ya dawa za mifugo pamoja na kuchukua hatua kwa wanaokiuka taratibu za uuzaji.
Kwa upande wake,Mkaguzi wa Dawa kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Venance Burushi, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea wafugaji uelewa juu ya matumizi sahihi ya dawa,ili kupunguza kasi ya usugu wa vimelea unaoweza kuhatarisha afya ya mifugo na binadamu.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, wakiwemo wadau wa ufugaji na wafugaji,wameeleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kufanya maamuzi sahihi wanapotumia dawa za mifugo, hivyo kuboresha uzalishaji na kuepuka madhara yanayotokana na matumizi yasiyo sahihi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za TMDA kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi bora ya dawa za mifugo na umuhimu wa kufuata ushauri wa wataalamu wa sekta hiyo.