
Mamlaka ya dawa na vifaa tiba ( TMDA) kanda ya Ziwa Mashariki imetoa onyo kali kwa wamiliki na wauzaji wa dawa baridi ambao wanajihusisha na utoaji wa huduma kama tohara, kulaza wagonjwa na kuchoma sindano kunyume na sheria na kanuni kuacha mara moja vitendo hivyo kwani vinahatarisha maisha ya wagonjwa
Akiwa katika semina maalum iliyoandaliwa na mamlaka hiyo wilayani Bariadi mkoani Simiyu na kukutanisha wamiliki na wauzaji wa dawa hizo ,Katibu wa Afya mkoa wa Simiyu Aziza Khamis amesema kuwa kujihusisha na huduma ambazo zilifaa kufanyika katika vituo vya afya na hospitali zinamfanya mgonjwa aweke rehani afya yake.

“Leo hii kuna baadhi ya maduka ya dawa wanafikia hatua hadi ya kulaza wagonjwa,kufanya tohara,sindano wanachoma vitu ambavyo vilifaa kufanyika hospitali huku ni kuchezea afya za watu,kwa hiyo kupitia semina hii ni imani yangu kubwa wadau hawa wakitoka hapa hawatokuwa kama walivyokuja” amesema Aziza
Akitolea ufafanuzi juu ya baadhi ya dawa ambazo ziko kinyume na sheria na miongozo kaimu meneja wa mamlaka hiyo Aggrey Muhabuki amesema kuwa tayari kuna orodha ya dawa zinazofaa kutolewa na maduka hayo kwa mujibu wa sheria japo kuwa bado baadhi ya maduka ya dawa hizo yanaziuza kinyume cha sheria
“Hatujalala na tunafanya ukaguzi kila mara kwa sababu zipo orodha za dawa ambazo zimeainishwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za afya zimeruhusu kutolewa na zilichapishwa katika gazeti toleo la serikali namba 63 lakini utakuta muuzaji anazo dawa hizo kazificha ndani anauza kiuficho,sasa tukimkamata mtu wa hivyo tunazichukua inakuwa hasara kwake na pia adhabu kali itafuata ikiwa ni pamoja na kulipa faini” amesema Aggrey.
Kaimu mfamasia mkoani humo Fillemon amesema kuwa zipo sheria na miongozo inayotakiwa kufuatwa na yeyote anayejihusisha na biashara ya kuuza dawa baridi hivyo kukiuka sheria hizo ni kujitafutia adhabu kali dhidi yako.
Penina Amos ni mmiliki wa duka la dawa kata ya Somanda wilayani Bariadi anasema kuwa moja kati ya changamoto wanazokutana nazo ni mgonjwa kufika dukani na kuchagua dawa anayoitaka bila kufuata ushauri
“Mimi ni muuzaji tu lakini mgonjwa anafika dukani anataka dawa ambayo ni tofauti na ugonjwa alioandikiwa na analazimisha kwamba hiyo ni dawa inayomsaidia,kwa wagonjwa waelewa unawashauri lakini wengine hata useme vipi sasa kwa kuwa sisi ni wafanyabiashara tunauza” amesema Penina.
Aidha wamiliki hao wameiomba mamlaka hiyo kuendelea kutoa elimu hadi vijijini ambako wakazi huwakosa wataalamu sahihi wa afya.
“Maeneo ya vijijini mara nyingi mke wa mwalimu huonekana msomi kuliko wengine,na hiyo hutumika kama fursa kwa wao kufungua biashara ya dawa muhimu niiombe mamlaka hii isiishie kwetu maana huko vijijni pia kuna uhitaji mkubwa” amesema James Luneja mmiliki wa famasi Bariadi mjini.


