THPS YATAMBULISHA MRADI ‘TANZANIA FAST HEALTH’ KUIMARISHA HUDUMA ZA VVU KAHAMA

Na Eunuce Kanumba, Kahama – Shinyanga.

Tanzania Health Promotion Support (THPS) imetambulisha rasmi Mradi wa Tanzania FAST Health katika Manispaa ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, unaolenga kuimarisha huduma za VVU kwa watoto, vijana, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha.

Mradi unatekelezwa na THPS kwa kushirikiana na Serikali, pamoja na Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na VVU (National Council of People Living with HIV – NACOPHA) na Mtandao wa Vijana Wanaoishi na VVU -Network of Young People Living with HIV (NYP+), kwa lengo la kuziba mapengo katika upimaji, utambuzi wa mapema, matibabu na mwendelezo wa huduma kwa watu wanaoishi na VVU.

Akizungumza wakati wa utambulisho wa mradi huo mjini Kahama  Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dr Honoratha Rutatinisibwa, amesema ujio wa FAST Health ni fursa muhimu kwa Serikali kuendelea kuimarisha huduma za VVU, hususan kwa watoto na vijana ambao bado wanakabiliwa na changamoto katika kufikiwa na huduma.

Dr Rutatinisibwa amesema kwa mujibu wa takwimu za Tanzania HIV Impact Survey (THIS) 2022–2023, kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi katika Mkoa wa Shinyanga ni takribani asilimia 5.6, hali inayosisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha kinga, upimaji, utambuzi wa mapema, matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa.

Amesema Mkoa wa Shinyanga umefanya vizuri katika kufikia malengo ya UNAIDS ya 95-95-95, ambapo umefikia asilimia 96.5, 99.2 na 98.9, lakini bado kuna haja ya kuendelea kuziba mapengo, hasa katika kuwafikia watoto na vijana.

Ameeleza kuwa baadhi ya changamoto bado ni kuchelewa kutambua watoto wenye VVU, upimaji kutowafikia watoto na wanafamilia wote wanaostahili, unyanyapaa, changamoto za usafiri na kiuchumi pamoja na baadhi ya wagonjwa kupotea katika mwendelezo wa huduma.

“Hakuna mtoto au kijana anayestahili huduma za VVU anayepaswa kuachwa nyuma. Tunapaswa kujua watoto wetu wako wapi, kuwafikia, kuwapima wanaostahili kupimwa, kuwaunganisha mara moja katika huduma pale wanapogundulika kuwa na VVU na kuwasaidia kufikia na kudumisha ufubazaji wa virusi,” amesema Dr Rutatinisibw

Amesema kupitia Mradi wa Tanzania FAST Health, Serikali inatarajia kuimarishwa kwa utafutaji hai wa watoto na vijana wenye VVU, ikiwemo matumizi bora ya index testing, kuongeza utambuzi wa mapema na kuhakikisha wanaobainika kuwa na VVU wanaunganishwa na huduma na matibabu.

Aidha, amesema mradi unapaswa kuimarisha huduma zinazomlenga mtoto, kijana na familia kwa ujumla, kuongeza ufuasi wa dawa na kuhakikisha watu wanaoishi na VVU wanaendelea na matibabu hadi kufikia na kudumisha ufubazaji wa virusi.

Dr Rutatinisibwa amesisitiza kuwa Mradi wa Tanzania FAST Health haipaswi kufanya kazi kama mradi unaojitegemea, bali inapaswa kuunganishwa kikamilifu katika mifumo ya Serikali ili matokeo yake yawe endelevu hata baada ya kipindi cha ufadhili kumalizika.

“RHMT, CHMT, vituo vya kutolea huduma za afya, THPS, jamii na wadau wengine tunapaswa kufanya kazi kama timu moja. Tunatarajia kila afua itakayotekelezwa iwe na umiliki wa Serikali na jamii, matumizi sahihi ya takwimu na mpango wa uendelevu,” amesema.Dr Rutatinisibwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi THPS, Dkt. Benedicta Masanja, akimwakilisha Mkurugenzi wa THPS, Dkt. Redempta Mbatia, amesema Mradi wa Tanzania FAST Health unalenga kutumia mbinu zenye ushahidi kuwafikia watoto, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na vijana wanaohitaji huduma za VVU na wale wanaoishi na VVU waendelee kupata huduma za matibabu.

Dkt. Masanja amesema mradi utatumia Mama Vinara 35, vijana rika na klabu za vijana katika kuongeza uelewa na kuwafikia wananchi, huku ukisisitiza umuhimu wa kupunguza unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na VVU.

Amesema utekelezaji wa mradi huo katika halmashauri ya Muheza na  Halmashauri ya Manispaa ya Kahama unalenga kuimarisha huduma zilizopo na kujenga mifumo endelevu kwa kushirikiana na Serikali, NACOPHA na NYP+.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi wa Tanzania FAST Health, Japhet Daud, amesema mradi huo umebuniwa kuchagiza utatuzi wa changamoto zilizopo katika huduma za VVU, ikiwemo unyanyapaa ambao bado unaendelea kuwa kikwazo kwa baadhi ya watu kujitokeza kupima, kuanza na kuendelea na matibabu.

Amesema moja ya malengo ya mradi ni kuboresha afya ya mama kwa kuwahamasisha wanawake wajawazito na wanaonyonyesha kuhudhuria kliniki, kuimarisha huduma za upimaji wa VVU kwa watoto na kuhakikisha watu wanaoishi na VVU wanaendelea kupata huduma na matibabu

Ameongeza kuwa jamii itaelimishwa kuhusu umuhimu wa watu wanaoishi na VVU kuendelea na matibabu na kufikia ufubazaji wa virusi, akisisitiza ujumbe kwamba mtu anayetumia dawa ipasavyo na kufikia kiwango cha virusi kutokomea mwilini haambukizi VVU kwa njia ya ngono.

Mradi wa Tanzania FAST Health ulianza Juni 2026 na unatarajiwa kukamilika Juni 2029, ukiwa tayari umetambulishwa katika Halmashauri ya Muheza mkoani Tanga, na sasa umetambulishwa rasmi katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *