Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema thamani ya mikopo inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeongezeka kutoka shilingi milioni 776 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 317 Juni mwaka 2023.
Mheshimiwa Majaliwa amesema mafanikio makubwa ni azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwainua wakulima wa Tanzania na kuendeleza Sekta ya Kilimo kwa ujumla.
Amesema hayo leo (Alhamisi Julai 06, 2023) wakati alipozindua Ofisi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania katika Kanda ya Kusini, Mtwara.
“Ukuaji huo umechagizwa na ongezeko la mtaji kutoka shilingi bilioni 61.09 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 302.01 katika mwaka 2022. Ninawapongeza sana kwa hatua hiyo kwani kadri mtaji unavyoongezeka na uwezo wa kuhudumia wakulima kwa njia ya mikopo unaongezeka”. Amesema Majaliwa
Akizungumza baada ya uzinduzi wa Ofisi hizo Mheshimiwa Majaliwa amewataka wananchi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma kuchangamkia fursa ya uwepo wa Ofisi hiyo ya Kanda Mtwara kupata uelewa zaidi kuhusu utaratibu wa kupata mikopo.
Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imetenga shilingi bilioni 35 kwa ajili ya mpango wa kuwakopesha wakulima wa korosho ili kuendeleza zao hili.