Jumla ya leseni 482 za nembo ya ubora ya TBS zimetolewa ambayo ni sawa na asilimia 53.6 ya lengo la kutoa leseni 900 kwa mwaka.
Akizungumza Bungeni Jijini Dodoma Waziri wa Viwanda na Biashara Seleman Jafo, wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2025/2026 ambapo amesema ,hadi kufikia Machi 2025, jumla ya nembo hizo za ubora za TBS zimetolewa.
“Miongoni mwa leseni hizo, leseni 205 zilitolewa kwa wajasiriamali wadogo wanaozalisha bidhaa mbalimbali kama vile siagi ya karanga, asali, maji ya kunywa, pombe kali (spirit), vifungashio, mchele na pombe,” amesema.

“Shirika limeendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali na wadau mbalimbali katika dhana nzima za kuzingatia mifumo ya ubora ili kuzalisha bidhaa zenye ubora,” amesema Jafo.
Amesema Wizara kupitia TBS imeendelea na huduma za kusajili majengo yanayohifadhi bidhaa za chakula na vipodozi kwa lengo la kuhakiki ubora na ufanisi wa maeneo hayo ili kuendelea kulinda afya za walaji.
“Hadi kufikia Machi, 2025, TBS imesajili majengo, maeneo ya uzalishaji, uuzaji na usambazaji wa bidhaa za chakula na vipodozi 10,923 ambavyo ni sawa na asilimia 84 ya lengo la kusajili na kutoa vibali 13,000 kwa mwaka. Kati ya maeneo yaliyosajiliwa, maeneo 8,748 yanajihusisha na chakula na maeneo 2,175 yanajihusisha na vipodozi,” mesema Jafo.
Hata hivyo, amesema hadi kufikia Machi, 2025, TBS imesajili bidhaa za chakula na vipodozi 1,672 ambavyo ni sawa na asilimia 79.6 ya lengo la kusajili na kutoa vibali 2,100 kwa mwaka. Kati ya bidhaa hizo, bidhaa 1,208 ni za chakula na bidhaa 464 ni za vipodozi.