TASAF YATOA ZAIDI YA MILIONI 300 KWA KAYA MASIKINI 5,723 UKEREWE

Zaidi ya Shilingi Milioni 300 zimetolewa na Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kwa kaya masikini 5,723 za Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza, ikiwa ni hatua ya kuzikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini uliokithiri.

Akizungumza wakati wa zoezi la uhawilishaji fedha kwa dirisha la kipindi cha Machi – Aprili 2025, Mwezeshaji kutoka katika mfuko huo wa maendeleo TASAF, Aziz Makongo amesema mfuko huo umekua na utaratibu wa kutoa elimu mbalimbali za msingi kwa walengwa ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha wahusika wanaelewa matumizi bora ya kipato chao na kuimarisha mazingira ya maisha yao ya kila siku.

Katika hatua nyingine Aziz amewataka walengwa wa TASAF wa kijiji cha Nkilizya kilichopo Kata ya Nkilizya kujitathimini juu ya mafanikio waliyoyapata kwa kipindi chote cha mradi, ili waweze kujua ni maboresho yapi wanatakiwa kuyafanya na kupiga hatua moja kwenda hatua nyingine.

Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Wilaya ya Ukerewe, Jenitha Damaseni amesema mfuko huo unatamani kuona kila mwananchi alieshiriki katika mradi huo anabadili maisha yake na hata kama mradi huo utaisha basi kila mmoja aweze kujisimamia mwenyewe.

“Tunataka kuhakikisha kuwa mpo tayari kuendelea na maisha hata baada ya mpango na kusherekea mafanikio mliyoyapata hata kama ni madogo angalau yameweza kukuvusha kutoka hatua moja hadi nyingine,” amesema.

Nao baadhi wa walengwa wa mradi huo akiwemo Maboga Bega, amesema mradi umemsaidia kukua kiakili kwa kuwa ameweza kukutana na wenzake wengi ambao wamekuwa wakiongea mara kwa mara nini wafanye angalau wakuze kipato chao na kujikwamua na umaskini uliokithiri.

“Tumefanikiwa kuunda vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana,kwa kiasi flani mradi huu umenifundisha kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha,niseme tu TASAF ni mkombozi wa wanyonge,” amesema Maboga.

Kwa upande wake Sophia Mataba ambaye pia ni mlengwa wa mpango huo katika kijiji cha Bukongo yeye anasema TASAF imemsaidia kujiimarisha kiuchumi kwani umemsaidie kupata fedha ambazo amezitumia kwa ajili ya kufanya shuguli ya ufugaji wa mbuzi.

“Nilianza bila kitu baadae nikanunua mbuzi wawili baada ya mwaka wakaanza kuzaliana nikaanza kuuza kwa ajili ya kupata pesa ya matumizi ya nyumbani mpaka sasa nimebaki na mbuzi saba.Pia nina wajukuu wanne ambao wote wanahudumiwa na TASAF kiafya na kielimu,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *