Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) linatoa taarifa kwa Umma kuhusu tukio la kuzama kwa boti ya uvuvi “MV LEGACY” yenye namba ya usajili DS/L1175 inayomilikiwa na Yakoub Juma Khamis na yenye urefu wa mita 11 na upana wa mita 1.7 iliyopatiwa
Cheti cha Usajili na Ubora na TASAC kufanya shughuli za uvuvi mnamo tarehe
06/03/2024.
Mnamo tarehe 10/03/2024 majira ya 10:01 alasiri, kituo chetu cha kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji (MRCC) kilipokea tarifa ya kuzama kwa boti ya uvuvi “MV LEGACY” iliyotokea majira ya saa 9:50 jioni karibu na fukwe ya Coco Beach, Msasani, Wilaya ya Kinondoni mjini Dar es salaam ambayo ilikuwa na jumla ya Mabaharia tisa (09) ikijumuisha Wavuvi sita (06), Mhandisi Mitambo mmoja (01) na Manahodha wawili (02).
Kituo cha MRCC kilifanya jukumu lake la kisheria la kuratibu shughuli ya uokoaji kwa kutoa tarifa kwa Jeshi la Polisi (Wanamaji) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kufanya juhudi za kufika eneo la tukio na kufanya zoezi la uokoaji. Watu wote tisa wamefanikiwa kuokolewa na wanaendelea vizuri kiafya bila ya kuwa na changamoto yoyote.
Boti hiyo ambayo ilikuwa katika majaribio ya kiufundi baada ya matengenezo ya mifumo ya uvuaji samaki kwa kukokota (Trawling), ilianza majaribio majira ya saa 3:00 asubuhi ikitokea maeneo ya Tandavamba, Kivukoni na kufanya majaribio ya kuvua samaki wakizunguka katika maeneo yenye maji mafupi karibu na eneo la daraja jipya la Tanzanite (Upanga) hadi Coco Beach (Oysterbay).
Ilipofika majira ya saa 9:50 Alasiri
wakati nahodha anabadilisha uelekeo wa boti kuelekea upande wa kulia ndipo kamba moja ya upande wa kushoto ikakatika na kusababisha uzito kelemea kwenye kamba ya upande wa kulia na ndipo uzito ulipohama ghafla na kuilazimisha boti kunywa maji upande wa kulia kisha kuzama.
TASAC inaendelea kutoa rai kwa amiliki na waendeshaji wa vyombo majini kuzingatia Sheria na Kanuni za udhibiti usafiri majini na kuhakikisha muda wote wanavalia majaketi okozi ili kujiepusha na maafa yanayoweza kusababishwa na tukio la ajali.