Clavery Christian, Bukoba – Kagera.
Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri Majini (TASAC), imefanya mkutano maalumu na wadau wa sekta ya usafiri majini, ili kujadili athari zinazotokana na kupanda kwa bei ya mafuta nchini Tanzania.
Akizungumza katika mkutano huo, Issaya Tendega katibu tawala msaidizi uchumi uzalishaji kwa niaba ya Katibu Tawala mkoa wa Kagera Stephen Ndaki amesema kuwa ongezeko la bei ya mafuta linaathiri moja kwa moja sekta ya usafiri majini, hali inayosababisha kupanda kwa nauli na gharama za usafirishaji wa mizigo.

Bwana Tendega amesisitiza umuhimu wa wadau wa usafirishaji majini kushirikiana katika kubuni mikakati ya kupunguza athari hizo ili kulinda uchumi wa wananchi na kuendeleza huduma za usafiri majini.
Wadau wa sekta hiyo wakiwemo wamiliki wa vyombo vya usafiri na watoa huduma bandarini wameeleza kuwa hali hiyo imekuwa changamoto kubwa kwao, wakidai kuwa baadhi yao wamelazimika kupunguza safari au kuongeza gharama kwa abiria ili kuendana na mabadiliko ya soko la mafuta.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa TASAC meneja uhusiano kwa umma Said Mkabakuli alieleza kuwa maoni ya wadau yote wameyachukua na wanaenda kuyafanyia kazi ili kuangalia uwezekano wa kuweka sera rafiki zitakazosaidia kupunguza mzigo kwa wadau wa usafiri majini.
Mkutano huo umefanyika kwa lengo la kutafuta maoni yenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili watoa huduma za usafiri majini, ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za uendeshaji wa vyombo vya usafiri ambazo zimeendelea kuongezeka kutokana na kupanda kwa bei ya nishati hiyo muhimu.



