TARURA YATAKIWA KUONGEZA KASI UKARABATI BARABARA ZA PEMBEZONI MWA MJI KASULU

Na Tryphone Odace, Kasulu – Kigoma.

Baraza la madiwani katika Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma, limeiomba Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuongeza kasi ya ukarabati na uboreshaji wa barabara za pembezoni mwa mji huo, ambazo zimekuwa na changamoto ya kupitika hasa kipindi cha masika.

Ombi hilo limetolewa wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026, kilichofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Fatima Laay, uliopo katika Halmashauri ya Mji Kasulu.

Sehemu ya Madiwani wakiwa katika kikao hicho.

Madiwani hao walisema hali mbaya ya baadhi ya barabara imekuwa ikiwakwamisha wananchi katika kutekeleza shughuli zao za uzalishaji mali kwa wakati, hususan usafirishaji wa mazao pamoja na upatikanaji wa huduma nyingine muhimu.

Ukiangalia barabara nyingi za mitaani hazipitiki kwani hazijakarabatiwa na hata zile zilikuwa zimeingia kwenye mpango wa kukarabatiwa ukarabati wake hauendelei kama barabara ya Mwilamvya na barabara mrufiti bado kabisa sasa tunasubiri hadi mvua zianze kunyesha tukarabati naona tutakuwa tumeshachelewa” walisema madiwani.

Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Kasulu, Mhandisi Eric Laban.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kasulu, Mbelwa Chidebwe, aliishauri Meneja wa TARURA kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya uboreshaji wa barabara katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo.

Chidebwe ametaja pia barabara inayoelekea kwa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu kuwa miongoni mwa barabara zinazohitaji kupewa kipaumbele, ili ziweze kupitika kwa urahisi na kuwezesha wananchi na watumiaji wengine kufika maeneo mbalimbali bila changamoto.

Wanaiomba Serikali kupitia TARURA, kuongeza kasi ya ukarabati na uboreshaji wa barabara za pembezoni mwa mji.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Kasulu, Mhandisi Eric Laban, amekiri kuwepo kwa changamoto ya uharibifu wa barabara katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo.

“Tunaendelea na jitihada za kukabiliana na changamoto hiyo, na hadi kufikia mwezi Septemba, wakandarasi wataendelea na utekelezaji wa kazi za uboreshaji wa barabara ili kuhakikisha mvua kabla hazijaanza kunyesha” alisema Eric.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kasulu, Mbelwa Chidebwe.

Naye mwakilishi wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Antony Lukole, amesisitiza umuhimu wa kutekelezwa kwa changamoto zote zilizowasilishwa na madiwani, ili kuboresha huduma kwa wananchi na kuwezesha shughuli za kiuchumi kuendelea kwa ufanisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *