TARIME WALIA UBOVU WA BARABARA TARIME-NYAMWAGA, WAOMBA USAIDIZI WA HARAKA

Wananchi wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kurekebisha Barabara ya Tarime-Nyamwaga, wakieleza kuwa hali yake imezidi kuwa mbaya na kusababisha ajali za mara kwa mara zinazohatarisha maisha ya watumiaji.

Ombi hilo linakuja kufuatia ziara ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, aliyefika wilayani Tarime pamoja na Serengeti kukagua hali ya miundombinu ya barabara katika maeneo hayo.

Wananchi wamesema kipande cha barabara kuanzia Jembe hadi Nyamwaga kimeharibika kiasi cha kushindwa kupitika kwa urahisi,hasa wakati wa mvua, hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa wasafiri na wafanyabiashara.

Dereva wa bajaji mjini Tarime, John Wambura, pamoja na wakazi wengine akiwemo Mwita Santuri na Casian John, wameeleza kuwa ubovu wa barabara hiyo umechangia ongezeko la ajali na gharama za matengenezo ya vyombo vya usafiri.

Akizungumza na wananchi hao, Waziri Abdallah Ulega amesema Serikali imejipanga kuchukua hatua za dharura, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mkandarasi anaanza kazi mara moja ili kurejesha hali ya barabara hiyo.

Katika hatua nyingine, akiwa eneo la Nyamwaga, Waziri Ulega aliwataka wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano, akisisitiza umuhimu wa kulinda umoja wa kitaifa huku naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Rhimo Nyanasaho, amewahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani, akieleza kuwa utulivu wa nchi ni msingi wa maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *