Na Gideon Gregory – Dodoma.
Mchakato wa kuziba pengo la uwakilishi wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), umeingia katika hatua ya mwisho kufuatia kutangazwa rasmi kwa uchaguzi mdogo utakaofanyika Mei 4, 2026 jijini Dodoma.
Uchaguzi huo unalenga kupata wajumbe watatu wapya baada ya nafasi hizo kubaki wazi kufuatia mabadiliko ya kisiasa ya baadhi ya wabunge waliokuwa wakilishika taifa katika chombo hicho cha kikanda.
Nafasi hizo zimeachwa wazi baada ya James Kinyasi Millya, Ng’waru Jumanne Maghembe na Angela Charles Kizigha kuingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatua iliyowafanya kisheria kupoteza sifa ya kuendelea kuwa wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki. Mabadiliko hayo yamelazimisha kufanyika kwa uchaguzi mdogo kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia Bunge.

Kwa mujibu wa Katibu wa Bunge, Baraka Leonard amesema uchaguzi huo unafanyika chini ya misingi ya kisheria ikiwemo Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Kanuni za Kudumu za Bunge, zinazotaka nafasi zilizo wazi kujazwa ndani ya muda wa siku 90.
Katika kuzingatia uwakilishi, nafasi hizo zimegawanywa katika makundi mawili ambapo nafasi moja ni ya wanawake (Kundi A) na mbili ni za Tanzania Bara (Kundi D). Mgawanyo huo unalenga kuhakikisha usawa na uwakilishi wa makundi mbalimbali kama inavyoelekezwa na sheria za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika hatua ya uteuzi iliyohitimishwa Aprili 30, 2026, wagombea watatu wameidhinishwa kushiriki uchaguzi huo. Fatuma Abdallah Kange anawania nafasi ya kundi la wanawake, huku Cosato David Chumi na Kambarage Masato Wasira wakichuana katika nafasi mbili za Tanzania Bara.
Siku ya uchaguzi, wagombea watapata fursa ya kujieleza mbele ya wabunge, kujibu maswali ya papo kwa papo na kuomba kura kabla ya zoezi la upigaji kura kuanza. Mfumo huo unalenga kuongeza uwazi na kuwapa wabunge nafasi ya kufanya maamuzi sahihi kwa kuzingatia uwezo wa wagombea.


