Tanzania na Rwanda zimekubaliana kushirikiana katika maeneo kadhaa ikiwemo kukuza biashara baina ya nchi hizo hasa baada ya kubainika kuwa kiwango cha biashara katika nchi hizo hakiendani na rasilimali za nchi hizo.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu aliyozungumza na Rais wa Rwanda, Paul Kagame Ikulu, Dar es Salaam. “Ziara hii imetupa muda mzuri wa kutathmini masuala yote ya ushirikiano kati ya nchi zetu mbili na kubuni mbinu mpya za mashirikiano zaidi,” alisema Rais Samia.
Alisema katika mazungumzo yao ya ndani viongozi hao walijadili na kukubaliana kuwa kuna haja ya kukuza biashara na kuweka miundombinu ya kukuza biashara kwa sababu kiwango cha biashara kilichopo hakiendani na rasilimali zilizopo katika nchi hizo ukizingatia uhusiano mzuri uliopo. Rais Samia alimweleza Rais Kagame kuwa Tanzania inaimarisha bandari zake hususani za Dar es Salaam na Tanga ambazo nchi hiyo inazitumia.
“Lakini pia tumezungumza kuangalia na kuimarisha njia nyingine za mawasiliano ili Tanzania itoe huduma kwa ufanisi kule Rwanda na nchi nyingine zinazotuzunguka,” alisema.