Na Ibrahim Rojala – Geita.
Tanzania imetajwa kuwa nchi kinara kwa kuwa na mwitikio chanya wa utekelezaji wa mradi wa majaribio wa uboreshaji wa mazingira na haki za mnyama Punda kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuitambua rasmi siku ya punda duniani ambayo inatarajiwa kufanyika Mei 8, 2026.
Meneja Mkuu wa Programu za Brooke East Africa, Elijah Mithigi ameeleza hayo akiwa mkoani Geita wakati akizungumzia mafanikio ya mradi wa majaribio uliolenga kuhakikisha mazingira salama ya kiafya kwa punda.

Amesema, Punda ni miongoni mwa wanyama waliosahaulika na mradi huo unaotekelezwa na shirika lisilo la Kiserikali la Arusha Society for the Protection of Animals (ASPA), kwa ufadhili wa Shirika la Brooke East Africa linalotekeleza shughuli zake katika nchi mbalimbali barani Afrika.
“We are very satisfied kwamba huu mradi umeanza vizuri na unaelekea vizuri,kuna mikakati ambayo tumeona lazima itiliwe mkazo,matandiko kwa mfano,kwahiyo bado kazi ipo,elimu bado tutazidisha,”

“Kuna maeneo ambayo hatujafika na tunajua yanahitaji kufikiwa lakini kwangu ambalo limenipatia furaha ni kuwa project imekwenda vizuri, malengo ambayo tulikuwa tumeyatarajia tumeanza kuona mwelekeo,” amesema Elijah.

Mkurugenzi wa Shirika la ASPA, Livingstone Masija ameeleza kwamba mnamo Mei 8,mwaka huu wamepanga kuadhimisha siku ya punda duniani ikiwa ni sehemu ya kuwaongezea watu uelewa wa kuhusu punda na umuhimu wake kutokana na kuwa na uwezo wa kufanya kazi mbalimbali kama vile kilimo,kutumiaka katika ujenzi na shughuli za migodini hususani mkoani Geita.
“Tunakuja Geita tarehe nane mwezi wa tano,Watanzania wote mnakaribishwa ili tuweze kufanya sherehe nzuri ya kumuenzi punda kama mdau mkubwa wa uzalishaji na ukuzaji wa uchumi nchini Tanzania,” ameeleza Masija.

Akieleza kuhusu mabadiliko yaliyopatikana wilayani Geita tangu kuanza kwa utekelezwaji wa mradi huo wa miaka mitatu, Afisa Mifugo kutoka ofisi ya mifugo wilaya ya Geita, Januari Masele amesema, kumekuwa na mabadiliko makubwa ikiwemo punda kutazamwa kama wanyama wengine ikiwa ni pamoja na kuwapatia huduma za matibabu,na kuchochea ongezeko la bajeti ya chanjo kwa halmashauri hiyo.

“Sisi kama halmashauri katika mwaka wa fedha 2026-2027 tumeongeza bajeti yetu ya chanjo kutoka milioni 30 mpaka milioni 50, lakini ndani yake humo tumemjumuisha mnyama punda,’ amebainisha Masele.


