Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UNTourism), limeitaja Tanzania kuwa nchi ilizoongoza Afrika kwa kuwa na ongezeko kubwa la watalii kwa mwaka 2024 ikilinganishwa na kabla ya janga la UVIKO-19 ambapo utalii Tanzania ulikua kwa asimilia 48, Ethiopia (40%), Morocco (35%), Kenya (11%) na Tunisia (9%).
Akizungumza leo Bungeni Jijini Dodoma Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Balozi Pindi Chana Wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 amesema, idadi ya watalii wa ndani waliotembelea vivutio vya utalii imeongezeka kwa asilimia 307.9 kutoka watalii 788,933 Mwaka 2021 hadi kufikia watalii 3,218,352 mwaka 2024.
“Idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 132.1 kutoka watalii 922,692 Mwaka 2021 hadi watalii 2,141,895”, amesema “Hatua hii imewezesha idadi ya watalii kufikia 5,360,247 sawa na asilimia 107.2 ya lengo la watalii 5,000,000 kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020”. Amesema Dkt. Chana.

Aidha amesema Mapato yatokanayo na shughuli za utalii yameongezeka kutoka
Dola za Marekani bilioni 1.3 Mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3.9 Mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 200 kwa watalii wa kimataifa.
“Aidha, mapato yatokanayo na utalii wa ndani yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 46.3 Mwaka 2021 hadi Shilingi bilioni 209.8 Mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 353.1”
“Hatua hii imeifanya Tanzania kuwa nafasi ya tisa (9) duniani na kushika nafasi ya
tatu (3) Barani Afrika kwa ongezeko la mapato ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya UVIKO-19”. Amesema Dkt. Chana