Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imejipanga vyema kukamilisha maandalizi yote muhimu ikiwemo miundombinu kwa ajili ya Michuano ya Mpira wa Miguu kwa Nchi za Africa CHAN na AFCON.
Majaliwa ameyasema hayo hii leo Februari Mosi, 2025 aliposhiriki katika Tamasha la Michezo la Bunge Bonanza lililofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin jijini Dodoma.

Amesema, “Tanzania imejipanga vizuri, kuhakikisha kuwa michuano hii inafanyika hapa Nchini, Serikali inawajibika kuhakikisha inaandaa viwanja na miundombinu mingine.”
Majaliwa ameongeza kuwa, tayari ukaguzi wa baadhi ya viwanja umefanyika na vimeonekana kukidhi vigezo upande wa Tanzania bara na Visiwani na kwqmba kazi bado inaendelea, lengo likiwa ni kuhakikisha michuano hiyo inafanyika kwa ufanisi.

Aidha, amesema ni vyema Watanzania wakajipanga kutumia fursa zitakazo jitokeza kutokana na kuwepo kwa michuano hiyo hapa Nchini. “Hii ni fursa kwetu Watanzania, lazima tujipange kutumia fursa za kiuchumi zitakazojitokeza, ili tuweze kunufaika”.
Waziri Mkuu pia amempongeza Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson kwa kuandaa Tamasha la Michezo la Bunge Bonanza ambalo limewakutanisha wabunge na wanamichezo mbalimbali wa Mkoani Dodoma.

“Tamasha hili limekuwa na mafanikio makubwa, limetupa nafasi wabunge kufanya mazoezi na kushiriki michezo mbalimbali pamoja na kuimarisha afya zetu,” alisema.
Ametumia nafasi hiyo pia kuwahimiza Watanzania kuendelea na utamaduni wa kufanya mazoezi, ili kuimarisha afya.
