Na Saada Almasi, Bariadi – Simiyu.
Kufuatia malalamiko ya watumiaji wa barabara inayounganisha wilaya ya Bariadi kwenda Lamadi, ambayo ndiyo njia pekee inayotumika kuunganisha mkoa wa Simiyu na mkoa wa Mara na Mwanza kuwa chakavu kwa muda mrefu, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoani Simiyu, imeendelea na marekebisho katika maeneo korofi, ili kuleta ahueni kwa watumiaji.
Mkandarasi Fabian Justine kutoka kampuni ya Mangi Construction Limited anayetekeleza marekebisho hayo yenye urefu wa kilometa 15 kwa gharama ya shilingi Bilioni 3.7 amesema kuwa utofauti uliokuwepo katika barabara ya awali yalitokana na kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha double surface ambacho baada ya kuchoka na kuleta mianya ilisababisha maji kupenya na haribu ubora wake.

Amesema, “kwa sasa tunaweka lami ambayo imechanganywa na kokoto na baada ya vipimo nya maabara imeonekana kufaa kuwekwa katika maeneo haya kwani kwa ubora wake si rahisi kuweka mashimo ambayo yanaweza kupitisha maji na pia yanahimili magari ya uzito ambao umeanishwa na TANROADS na kwa kiwango hiki inauwezo wa kudumu kuanzia miaka mitano hadi ishirini hivyo kuwahakikishia watumiaji usalama wao na vyombo vyao.”
Kwa upande wake meneja wa TANROADS Mkoani Simiyu, Boniface Mkumbo ameiambia jambo Fm hatua hiyo inatokana na ahadi yake aliyoitoa katika kikao cha bodi ya barabara miezi miwili iliyopita kilichoketi mjini Bariadi ambapo aliahidi kuanza marekebisho ya maeneo yote korofi.

“Tayari serikali yetu imetupatia pesa za kukarabati na faida yake ni kwamba baada ya matengenezo magari yenye uzito mkubwa yanaweza kupita bila shida ukizingatia mkoa wa Mara,Mwanza na Simiyu kuna shughuli nyingi za kiuchumi zitarahisishwa na barabara pia kwa ubora huu haiwezi kupitisha maji kwa hiyo tusitegemee itaharibika haraka na hapa tupo eneo la Nanenane tunaelekea Dutwa na baadae Sapiwi ambako kuna hatari zaidi” alisema Mhandisi Mkumbo.
Ameongeza kuwa, ”nitoe rai kwa wananchi walio kando na barabara tumekuwa na shughuli nyingi za kiuchumi kama kupitisha mifugo barabarani ,kuchota mchanga kando na barabara na hata kukokota matrekta sasa tutambue kuwa tunachangia sana kuharibu barabara zetu yatupasa tusitishe shughuli hizo mara moja ili tutumie barabara kwa muda mrefu.”

Kufuatia hatua hiyo ,Jambo Fm ilitaka kujua mapokeo ya ukarabati huo, ambapo Paul Majira Dereva wa daladala kutoka Bariadi kwenda Lamadi alisema mashimo ya barabara hiyo yalimgharimu kufanya marekebisho ya magurudumu ya gari lake, kwani wakati mwingine yalipasuka ghafla mara baada ya kukita kwenye shimo.
“Magari tunayafanyia marekebisho kila baada ya muda mfupi haijalishi umeweka magurudumu mapya ama ya zamani ,kuna kipindi unaweza kukwepa shimo ukagongana na gari jingine na kuleta ajali kwa sababu shimo umeliona ghafla na unalazimika kulikwepa na kuna maeneo mabaya zaidi kama kutoka Sapiwi hadi Dutwa usipo kuwa makini unapata ajali mbaya kwa haya marekebisho tunaishukuru sana serikali yetu,” amesema Paul.
“Sisi wasafiri tunatumia muda mrefu zaidi wa safari kwa kuwa sisi ni wakulima na wafugaji tunahitaji barabara kwa ajili ya kusafirisha mazao yetu na pia tufike kwa wakati, lakini kutokana na barabara ilivyokuwa chakavu tulilazimika kuchelewa kufika sokoni kwa sababu ya kukwepa mashimo, ninaiomba Serikali kuendelea kurekebisha, ili maeneo yote chakavu yapate kupitika kwa urahisi na salama,” alisema Moshi Jumbo.