TANROADS yafunga taa 300 Geita

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Geita umetekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha maeneo ya miji katika barabara za TANROADS yanawekewa taa za barabarani ambapo katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Tanroads Mkoa wa Geita imeweka taa za barabarani 300 zenye urefu wa kilomita 5 katika miji ya Geita na Katoro.


Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Geita Mhandisi Ezra Magogo ameeleza hayo wakati akizungumza na Jambo Fm na kufafanua kuwa Mkoa wa Geita una mtandao wa barabara za lami Kilomita 400.98 sawa na asilimia 39 ya mtandao wote wa barabara ambapo taa hizo 300 zimewekwa katika mji wa Geita, Katoro na maeneo mengine ili kuongeza usalama pamoja na kuwawezesha wajasiriamali kufanya biashara usiku na mchana.


Mkuu wa kitengo cha Matengenezo TANROADS Mkoa wa Geita Fredrick Mande amesema licha ya serikali kutumia fedha nyingi kutengeneza taa za barabarani lakini bado baadhi ya wananchi wamekuwa wakiharibu taa hizo hasa madereva ambao mara mingi wamekuwa wakigonga taa hizo na kuziharibu.


Nao baadhi ya wakazi wa Mji wa Geita na Mji mdogo wa Katoro wamesema uwepo wa taa hizo za barabarani katika maeneo yao kumesaidia kupunguza matukio ya uhalifu yaliyokuwa yamekithiri pamoja na kuwasaidia wajariliamali kufanya biashara zao usiku na mchana hali ambayo inasaidia kukuza uchumi wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *