Na Cecilia Shiratu, Muleba – Kagera.
Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), limewataka Wananchi Wilayani Muleba mkoani Kagera, kushirikiana na vyombo vya usalama katika kutoa taarifa za watu wanaohusika na wizi, uharibifu na hujuma dhidi ya miundombinu ya umeme, ikiwemo nyaya za shaba na Transfoma.
Afisa Usalama wa TANESCO Mkoa wa Kagera, Philipo Mwingira amesema, baadhi ya Wananchi wasio waaminifu wamekuwa wakihusika katika vitendo vya kuhujumu miundombinu ya umeme kwa kuiba nyaya za shaba, hivyo kulisababishia shirika hasara na kuwaacha Wananchi bila huduma ya umeme.
TANESCO, imeamua kuwashirikisha Wananchi kwa pamoja katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo, kwani baadhi yao wamekuwa wakitoa taarifa zinazosaidia kubaini watu wanaohusika na wizi wa miundombinu hiyo.

Kwa upande wake, Afisa Usalama wa TANESCO Mkoa wa Geita, Eleuterias Katemana amesema kikao hicho kimelenga kutoa elimu kwa Wananchi kuhusu kudhibiti wizi na uharibifu wa miundombinu ya umeme, pamoja na kujenga ushirikiano kati ya wananchi na TANESCO.
Amewataka Wafanyakazi hao kuwa na vitambulisho, ili kuondoa uwezekano wa watu wasiohusika kujitambulisha kama watumishi wa shirika.
Katemana amesema, usalama wa miundombinu ya umeme ni jukumu la pamoja, kwani wananchi ndio wanaoathirika zaidi pale miundombinu inapoharibiwa au kuibiwa.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano Wilaya ya Muleba, Sadam Salai amesema maeneo yaliyoathirika zaidi na wizi wa miundombinu ya umeme ni pamoja na Kamachumu, Izigo, Nshambya.
Salai amesema, mwaka 2023 transfoma zaidi ya 50 ziliibwa, mwaka huu 2026 tayari transfoma 19 nyaya za shaba, nguzo na mita za umeme zikiibwa.
Amesema, vitendo hivyo vimekuwa vikisababisha baadhi ya wananchi kukaa bila umeme kwa muda mrefu, huku baadhi ya maeneo huduma ya umeme ikikatika kutokana na miundombinu kuibwa au kuharibiwa.

Afisa Usalama mkuu uzuiaji TANESCO Makao Makuu, Shami Dunia amesema kutokana na changamoto iliyopo amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za siri kuhusu watu wanaojihusisha na wizi au uharibifu wa miundombinu ya umeme.
Shirika hilo, limeanzisha mfumo wa kupokea taarifa kwa siri bila kumtambulisha mtoa taarifa, ambapo Wananchi wanaweza kupiga simu kupitia namba 180 na kutoa taarifa kuhusu vitendo vya wizi, uharibifu au hujuma dhidi ya miundombinu ya umeme.


