TANESCO MBIONI KUANZISHA MKOA MAALUM MRADI WA SGR

Na Gideon Gregory – Dodoma. 

Shirika la umeme Nchini (TANESCO) limesema lipo mbioni kuanzisha  Mkoa  maalum kwa ajili ya mradi wa Reli ya kisasa kwa kiwango cha mataifa (SGR) ili kuimarisha utoaji wa huduma za safari ya treni.

Kauli hiyo imetolewa leo Machi 26,2025 hapa Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi Gissima Nyamo -Hanga wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita. 

Aidha amesema kuwa hali ya uzalishaji umeme kwenye gridi ya Taifa imeongezeka mara mbili zaidi baada ya kutekeleza miradi ya ufuaji umeme maeneo mbalimbali nchini.

“Baada ya kukamilika kwa miradi ya uzalishaji umeme hadi Februari mwaka huu uwezo wa mitambo ya kufua umeme kwenye gridi ya Taifa umefikia megawati 3,796.7, wakati mahitaji ya juu ya umeme kwenye mfumo wa gridi umefikia megawati 1,908. 

“Mwaka 2021 uwezo wetu wa kuzalisha ulikuwa megawati 1,573.6 na sasa hivi uzalishaji umeongezeka zaidi ya mara mbili ya uwezo wa kuzalisha umeme kwa kipindi kifupi cha miaka minne,” amesema.

Amesema mafanikio hayo yamechangiwa na miradi kama Bwawa la Mwalimu Nyerere la mitambo tisa lenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, mradi wa megawati 80 wa Rusumo, mradi wa gesi asilia wa Kinyerezi 1, wa megawati 185 pamoja na mradi wa jua Kishapu Shinyanga wa megawati 150 unaoendelea.

“Uwezo wa vinu vya kufua umeme ni megawati 3,796.7  lakini matumizi ya watanzania mpaka sasa ni megawati 1,900 na mfano wake ni kama gunia la unga ndani, umepata mshahara ukasema pesa inaweza ikaisha kwa hiyo unanunua gunia la unga unaweka ndani ili uwe unachota kidogo kidogo unatumia mpaka mwezi uishe, ndivyo umeme ulivyo”.

Amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.

Amesema wanaposema kuna umeme mwingi unaozalishwa maana yake unakaa kama akiba na unakuwa unavutwa kulingana na mahitaji.

Pia ameongeza kuwa kuna mradi unajengwa wa laini kubwa ya umeme ya msongo wa Kilovati 400 ambayo itabeba umeme kutoka Chalinze (Pwani) kwenda Dodoma, na umeme huo utasafirishwa kupitia laini hiyo kwenda kituo cha kupoza umeme (Substation) cha Zuzu kilichopo Jijini Dodoma ambacho ndicho kituo mama kutoka kwenye mfumo wa Gridi ya Taifa.

Amesema mradi huo muhimu ambao unafadhiliwa na Serikali, umeanza kutekelezwa katika awamu ya sita chini ya uongozi ya Rais Samia Suluhu Hassan. 

Mradi huo umefikia asilimia 15 ya utelelezaji wake na unatarajiwa kukamilika mwaka 2026, na kwamba ndio muarobaini wa changamoto nyingi za umeme ambazo zipo kwa sasa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *