TAMADUNI YA MBINA NA DHANA YA UPONYAJI MARADHI, HUTUMIKA PIA KUFIKISHA UJUMBE KWA JAMII

Na Saada Almasi – Simiyu.

Mbina ni utamaduni wa Ngoma katika jamii ya Kisukuma ambayo hufanyika mara baada ya mavuno na kujumuisha watu wa kabila hilo katika sherehe ya pamoja

Ilianza kufanyika miaka ya 1970 na hadi sasa bado inaenziwa huku matukio makubwa ambayo hufanyika yakiwa ni ngoma na matukio ya kijadi yanayo pambwa na mgawanyiko wa makundi mawili ya kikabila yaani kundi la chifu ambalo ndani yake kuna Wagika na Mihongo lenye Wagalu ambao hushindana kwa kucheza na uganga wa jadi.

Sherehe za mbina hufanyika kila kata ya mkoa wa Simiyu lakini jumuisho kubwa hufanyika kila siku ya 5 ya mwezi wa sita ambapo watu wa kabila hili kutoka kila pembe ya nchi hukutana kuienzi 

Kata ya Kasoli kijiji cha Mwamlapa wilayani Bariadi ndiko mwenyeji wa mbina hii kimkoa ambapo Diwani wa Kata hii ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Mayalla Lucas anasema kuwa Serikali hutumia jumuiko hili kufikisha ujumbe wa kimaendeleo 

“Siku za hivi karibuni watu huwa hawajitokezi kwa wingi katika mikutano kutokana na hilo pale ambapo kunakuwa na mkusanyiko mkubwa hivi ndio tunatumia kufikisha ujumbe wa serikali hususan mwaka huu wa uchaguzi mkuu tumehamasisha watu kujitokeza kupiga kura na kuitunza amani ya nchi,” amesema Mayalla.

Ameongeza kuwa mbina ya mwaka 2022 ilibeba ujumbe unaohamasisha watu kujitokeza katika zoezi la sensa,lakini 2024 ililenga ujumbe kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Jamii ya hapa inathamini utamaduni kwa hiyo wanapoitana pamoja wanakula pamoja hata yule ambaye huwa hatoki kwake siku hiyo utamuona na ndipo ujumbe wa kimaendeleo unapofikishwa maana kila mtu yupo hata mtoto atajua,” alisema.

Joseph Ngalu ni mmoja wa wahudhuriaji wa mbina ya Kasoli, anasema kuwa baadhi yao hutumia kama fursa ya kibiashara kwa kuleta bidhaa zao na kwa kuwa watu hutoka kwenye mavuno biashara huchangamka

“Ukitembea huko utaona watu wengi kila mmoja na biashara yake watu wako hapa tangu asubuhi lazima ale hapa ndiyo maana mama lishe anauwezo wa kuchinja mbuzi zaidi ya kumi na akauza chakula kikaisha,na bado wenye nguo,matunda maji wote wako hapa,” amesema Joseph.

Inasemekana unapokuwa umehudhuria mbina basi una uhakika wa ugonjwa unaokusumbua kuisha kwani mbali na burudani zipo dawa ambazo watu hukanyaga na kumwagiwa maji maalum ambayo yanasadikika kuondosha magonjwa kama kuvimba miguu na hatimaye ugonjwa kuishia pale.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *