Na Ibrahim Rojala – Geita.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Francis Chalamila ametoa wito kwa watumishi wa TAKUKURU wanaofanya kazi katika wilaya zenye majengo mapya kuhakikisha wanayatunza majengo hayo pamoja na vitendea kazi, ili viweze kutumika hata kwa viziazi vijavyo na kuleta ufanisi mkubwa na kuwataka wananchi kuzitumia ofisi za taasisi hiyo katika mapambano dhidi ya rushwa.
Ametoa agizo hilo wakati akizindua jengo la ofisi za TAKUKURU, Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita lililojengwa kwa tahamani ya zaidi ya shilingi milioni 386 na kuzitaka halmashauri nchini kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa viwango vya juu na kwa ubora, kuongeza uwazi kwa kuhakikisha zinaweka utaratibu wa kuwatangazia wananchi, kwa kubandika katika mbao za matangazo miradi yote iliyopitishwa katika halmashauri husika.

‘Ni azma ya TAKUKURU kuona kuwa miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kiwango cha juu cha ubora na katika hilo tunashauri kila halmashauri iweke utaratibu wa kuwatangazia wananchi kwa kubandika katika mbao za matangazo miradi yote iliyopitishwa katika halmashauri husika utaratibu huu ni muhimu katika kuongeza uwazi na uwajibikaji na hivyo kuziba mianya ya rushwa na kuongeza ushiriki wa wananchi katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa ipasavyo,” ameeleza Chalamila
Aidha ametoa wito kwa shule zote za msingi na sekondari mkoani Geita ambazo hazijafungua klabu za wapinga rushwa kufanya hivyo, viongozi wa dini, vyama vya siasa na vyama vya kijamii kushiriki katika kukataa na kupinga vitendo vya rushwa na kuwataka wananchi kushiriki katika zoezi la kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Geita, James Ruge amesema kukamilika kwa jengo hilo kunatarajia kuongeza wadau wa mapambano dhidi ya rushwa kutokana na uwepo wa mazingira rafiki katika jengo hilo na kuongeza ari ya utendaji kazi kwa watumishi wa taasisi hiyo katika wilaya ya Nyang’hwale kutokana na mazingira na miundombinu ya ofisi hiyo mpya kuwa rafiki.
‘Matarajio yetu baada ya jengo hili kuzinduliwa ni kuongezeka kwa wadau katika kuzuia na kupambana na rushwa kwani mazingira ya ofisi hii ni rafiki kwa kila mdau lakini pia ari ya watumishi kufanya kazi itaongezeka zaidi ya kuwa na mazingira rafiki na mzingira rafiki katika kuwatumikia wananchi wa Nyang’hwale na watanzania kwa ujumla’amesema Ruge.

Sarah Robert Lusana na Daudi Nyanda ambao ni baadhi ya wananchi walioshiriki uzinduzi wa jengo hilo wameipongeza serikaliwakieleza kwamba awali taasisi hiyo ilikuwa katika jengo la kupanga lisiloendana na hadhi yake wakiongeza kuwa litawasaidia kukaa imara na kulitumia kujifunza mambo mengi yanayohusu mapambano dhidi ya rushwa.



