Na Daniel Gahu – Katavi.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi, katika robo ya pili iliyoanzia Oktoba hadi Desemba, 2025 ilifanikiwa kuokoa kiasi cha Shilingi za Kitanzania 29,994,982/= kupitia kazi za uzuiaji rushwa, uchunguzi, mashaka na kusaidia kuongezeka Kwa mapato ya Halmashauri.
Ripoti hiyo, imetolewa na Naibu Kamanda Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Stewart Kiyondo akisema Shilingi 12,000,000/= zilirejeshwa baada ya kubainika kuwa mikopo ya asilimia 10 iliyotolewa na Halmashauri ya Mpimbwe kwa kikundi cha wanawake ilitumika kinyume na malengo yaliyokusudiwa.
“Baada ya ufuatiliaji wa TAKUKURU, fedha hizo zilirejeshwa na kuwekwa katika akaunti ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu mnamo tarehe 25 mwezi November, 2025,” alisema Kiyondo.

Amesema, pia Shilingi 17,994,982.19 zilirejeshwa kupitia hatua za uchunguzi na mashtaka zilizochukuliwa baada ya washtakiwa katika mashauri mbalimbali kuingia makubaliano ya kisheria (Plea Bargaining).
Fedha hizo, zilihusisha mapato ya ndani yaliyo kusanywa kupitia mfumo wa POS na kutokuwasilishwa benki zimewasilishwa katika akaunti ya Deposit ya Halmashauri ya wilaya ya Mlele kwa ajili ya utendaji wa miradi ya Maendeleo na huduma kwa wananchi.
Katika kipindi tajwa, miradi 6 inayotekelezwa katika Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika yenye thamani ya Shilingi 544,666,194/= ilibainishwa kuwa na mapungufu na kuyafanyia kazi mapungufu hayo.

Ufuatiliaji wa TAKUKURU umesaidia kudhibiti na kuweka uwazi katika usimamizi wa vifaa vya utekelezaji wa miradi hiyo.
Awali, TAKUKURU ilifuatilia matumizi ya Shilingi 1,634,374,369.00/= za utekelezaji wa miradi ya Maendeleo 12 katika sekta za Elimu, Afya na miundombinu ili kuhakikisha thamani ya fedha iliyotolewa inaendana na utekelezaji wa miradi.

Aidha katika kipindi chote cha uchunguzi wananchi wamepata uelewa zaidi kuhusu rushwa na madhara yake na namna wanavyoweza kushirikiana na Serikali katika kudhibiti vitendo vya rushwa katika maeneo yao.
Katika upande mwingine Kaimu Kamanda Mkuu amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika ufuatiliaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo ndani ya maeneo yao kwani miradi yote inayoanzishwa na Serikali ni nguvu za wananchi kwa asilimia miamoja na wanufaika namba moja ni wananchi wenyewe.
