Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoani Simiyu imefanikiwa kunusuru zaidi ya milioni 500 katika Mradi wa ujenzi wa shule ya Amali Kundo iliyopo Kata ya Nkololo Wilayani Bariadi.
Akitoa taarifa ya robo mwaka, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Simiyu, Aaron Misanga amesema pesa hizo zilitakiwa kutumika katika kununua vifaa vya ujenzi wa madarasa nane, Maabara mbili za Kemia na Baiolojia, Jengo la Maktaba, Nyumba moja ya Mtumishi, kichomea taka na matundu ya vyoo 10.
“Lakini kutokana na uzembe wa usimamizi kutoka kwa mkandarasi na fundi mkuu vifaa vilivyonunuliwa vikawa chini ya kiwango hali ambayo ingeitia hasara serikali wakati wa ufuatiliaji na kuna uzembe ambao tuliubaini kufanyika ikiwa ni pamoja na mchanga uliojaa tope kutumika kufyatulia tofali ambazo si imara,” alisema.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Screenshot_20250212-193606_Chrome.jpg)
Misanga ameongeza kuwa, “Saruji kutunzwa katika mazingira yasiyo salama ambayo yangeitia hasara Serikali na yote hayo ni kutokana na kutokuwepo kwa fundi na Mkandarasi muda mwingi eneo la mradi.”
Amesema, kutokana na ukaguzi wa ubora wa vifaa uliofanyika Taasisi ilijiridhisha na kutoa agizo la kusitishwa shughuli za ujenzi hadi pale wahusika watakapo timiza wajibu wao ikiwa ni pamoja na mifuko 480 waliyoiagiza kutoka kampuni ya saruji ya Dangote yenye thamani ya zaidi ya milioni 10 ambayo hadi sasa haijafika na hakukuwa na ufuatiliaji wowote.
“Baada ya kubaini uzembe huo tuliwataka kusitisha shughuli za ujenzi hadi pale watakapo timiza wajibu wao sambamba na kufuatilia saruji ambayo ina thamani ya zaidi ya milioni kumi ambayo haikuwa na ufuatiliaji wowote,” alisema Misanga.
Aidha, Taasisi hiyo imeendelea kutoa elimu kuhusu mapambano ya rushwa hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kwa wadau mbalimbali kupitia programu ya TAKUKURU RAFIKI, li kuifanya jamii kuendelea kuwa na mwamko wa kutoa taarifa za viashiria vya rushwa katika maeneo yao.
“Tunawashukuru wananchi wa mkoa wa Simiyu kwa kuendelea kutupatia taarifa za viashiria vya rushwa na sisi kupitia program yetu ya TAKUKURU RAFIKI tutaendelea kutoa elimu kwa makundi yote katika jamii ili muendelee kuwa na mwamko zaidi wa kutoa taarifa na hatimaye tuyatokomeze,” alibainisha Misanga.