TAKUKURU SHINYANGA YAFANIKISHA KUKAMILIKA KWA ZAHANATI YA SONGAMBELE

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoani Shinyanga, imefanikisha ukamilishaji wa Zahanati ya Kijiji cha Songambele Wilayani Shinyanga, baada ya kufuatilia matumizi ya shilingi milioni 26 zilizotolewa na Serikali.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy amebainisha hayo hii leo Septemba 3, 2025  wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo  kwa kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu kwa waandishi wa habari kupitia program ya Takukuru Rafiki.

Amesema, Fedha hizo zilizotolewa kupitia Mfuko wa Jimbo, ambazo zilikaa zaidi ya miezi mitatu katika akaunti ya Kituo cha Afya Salawe bila kutumika kwa kazi ya ukamilishaji wa Zahanati hiyo, hali iliyosababisha Wananchi kuendelea kukosa huduma za matibabu.

Kessy ameongeza kuwa, Wananchi wa Kijiji cha Songambele walijitolea nguvu kazi kujenga Boma la Zahanati zaidi ya miaka 16 iliyopita, lakini halikukamilika, hata baada ya Serikali kutoa Shilingi Milioni 26.

“Tulifuatilia fedha hizi kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, na kuweka mikakati ya kuhakikisha zitatumika kukamilisha zahanati hiyo,” amesema Kessy.

Aidha, amesema fedha hizo zilitolewa kwenye akaunti ya Kituo cha Afya Salawe, na zikatumika kununua vifaa vyote muhimu, na sasa wananchi wanapata huduma za matibabu.

Kessy ameongeza  kuwa, kwa kipindi hicho pia wamefanikiwa kuzuia mianya ya rushwa kwenye miradi 11 ya maendeleo yenye thamani ya Bilioni 3.5, baada ya kubaini kasoro ambazo zingesababisha kujengwa chini ya kiwango.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *