Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi ya fedha taslimu Shilingi Bilioni 1, iwapo Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) watafanikiwa kutwaa Ubingwa wa CHAN 2024 ambayo yanafanyika mwaka huu (2025), kwa pamoja katika mataifa matatu ya Tanzania, Kenya na Uganda.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Palamagamba Kabudi amesema Rais Samia ametoa ahadi hiyo endapo Taifa Stars itatwaa ubingwa huo wa CHAN 2024.
“Katika kuchagiza hamasa kwa timu yetu ya Taifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa ahadi ya donge nono Shilingi Bilioni 1 kwa vijana wetu wa Taifa Stars wakifanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano haya ya CHAN 2024,” amesema Prof. Kabudi.

Amesema, Tanzania haijapata nafasi hiyo kwa bahati mbaya, bali ni kutokana na uwekezaji na hamasa ya Rais Samia katika uwekezaji kwenye sekta ya michezo.
Ameongeza kuwa, maandalizi mengine muhimu ya mashindano hayo yameshafanyika ikiwemo maandalizi ya mchezo wa ufunguzi, kufanya malipo ya gharama za ada, maandalizi ya viwanja vya mashindano pamoja na mazoezi.
Ametoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa za kibiashara na uchumi ikiwemo vyakula malazi na usafirishaji kwa wakati huu wa mashindano ya CHAN.
Kwa upande wa hamasa Waziri amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi katika kuishangilia timu ya Taifa kama kaulimbiu iliyozinduliwa katika Uwanja wa Zakhiem Mbagala ya LINAKUJA NYUMBANI.

Pia kutakuwepo na hamasa kubwa kwa siku mbili kabla ya mashindano ambapo kutafanyika tamasha la muziki wa Singeli litalalojulikana kama CHAN SINGELI FESTIVAL kwa lengo pia la kuhamasisha muziki huo kimataifa.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerson Msigwa amesema kutakuwepo na zawadi ya goli la mama ambapo itatoka zawadi ya Milioni 10 kwa kila goli watakalofunga Taifa Stars katika michezo ya makundi na mtoano na zawadi itapanda hadi shilingi millioni 20 kwa kila goli watalalofunga kwenye mechi za nusu fainali na fainali.
Mchezo wa ufunguzi wa mashindano hayo utafanyika Agosti 2 katika Uwanja wa Benjamini Mkapa Jijini Dar es Salaam, ambapo timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itashuka dimbani kucheza na Burkina Faso na mgeni rasmi wa mchezo huo anatarajia kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
One response to “TAIFA STARS KULAMBA BILIONI 1 YA RAIS SAMIA WAKITWAA UBINGWA WA CHAN”
Hey there, jambofm.co.tz is yours…