Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Dkt. John Pima amesema Kata ya Ndevelwa imekuwa mfano wa kuigwa katika ushiriki na kujitolea kwa wananchi kwenye miradi ya maendeleo.
Dkt. Pima ametoa pongezi hizo wakati wa ziara ya Menejimenti ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo ya Manispaa.

Akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Inala, Kata ya Ndevelwa, Dkt. Pima amewapongeza wananchi hao kwa kujitolea na kushirikiana katika ujenzi wa ofisi ya kijiji, akisema ushiriki huo ni mfano mzuri wa wananchi kuchangia maendeleo yao.
Katika ziara hiyo, Menejimenti imetembelea na kukagua Shule ya Sekondari Uledi, Kituo cha Afya Mailitano, Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Itonjanda, Zahanati ya Manoleo pamoja na Ofisi ya Kijiji cha Inala katika Kata ya Ndevelwa.

Ametoa wito kwa wananchi wote wa Manispaa ya Tabora kuendelea kujitolea na kushiriki katika miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa Serikali pekee haiwezi kutekeleza kila jambo bila ushirikiano wa wananchi.
Dkt. Pima pia ameridhishwa na utekelezaji wa miradi yote ya afya iliyotembelewa katika ziara hiyo huku akisisitiza kuwa kila idara inapaswa kutekeleza wajibu wake kwa wakati ili kuhakikisha miradi inakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Amezielekeza idara wezeshi kuhakikisha zinatimiza wajibu wao kwa wakati, huku idara za ushauri zikitoa ushauri wa kitaalam unaohitajika katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Kwa upande wa Idara ya Manunuzi, Dkt. Pima amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi yote iliyopangwa kutekelezwa mwaka 2026 inatangazwa kwa wakati, ili kuwezesha kupata wazabuni mapema na hivyo kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Ziara ya Menejimenti inaendelea na inalenga kukagua maendeleo ya miradi, kubaini changamoto na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa ili miradi ikamilike kwa wakati na kutoa huduma zinazokusudiwa kwa wananchi.



