TABORA: CHALAMILA AWAPA NENO WAKUU WA TAKUKURU WILAYA

Pascal Tuliano – Tabora.

Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini, Chrispin Chalamila ametoa wito kwa Wakuu wa Taasisi hiyo ngazi ya Wilaya kuendelea kutunza miundombinu hususan majengo mapya yanayojengwa katika maeneo yao.

Chalamila ametoa Rai hiyo, 2025 wakati wa uzinduzi wa jengo na Ofisi mpya ya TAKUKURU Wilayani Kaliua, shughuli ambayo imehudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Dkt. Gerald Mongella.

Katika hotuba yake, Chalamila amewasisitiza wadau na watendaji katika sekta ya umma kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa maendeleo ya taifa ili kuongeza uwazi na uwajibikaji ndani ya jamii.

“Hatua hii ni muhimu sana ili kuongeza ufanisi, haki na usawa katika utekelezaji wa majukumu bila upendeleo katika jamii.” Amesema Chalamila.

Pia ametoa rai kwa shule zote za msingi na Sekondari nchini kuwa na vilabu vya wapinga rushwa katika jamii pamoja na Skauti.

Amesisitiza pia jukumu la wananchi katika kutunza jengo hilo na kulitumia katika kupinga na kuripoti vitendo vya rushwa wilayani humo.

“Jukumu la kila mwananchi wa wilaya ya Kaliua ni kulilinda jengo hili na kulitumia kikamilifu katika harakati za kupinga vitendo vya rushwa katika jamii.” Ameongeza Chalamila.

Kuelekea uchaguzi mkuu, Chalamila ametoa rai kwa wananchi kujiepusha na wagombea wasio waadilifu wanaotoa rushwa katika kipindi hiki cha kampeni na uchaguzi mkuu.

“Msiuze utu wenu kuelekea uchaguzi mkuu, mjitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura lakini kuweni makini sana na viongozi wanaotoa rushwa ili muwachague siku ya uchaguzi.” Amesisitiza.

Mradi wa jengo hilo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Kaliua ulianza kutekelezwa mwezi Januari 2025 na kukamilika Septemba 8, 2025 ukiwa umegharimu zaidi ya Shilingi milioni 373 za Kitanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *