Serikali Mkoani Mwanza, imewataka Viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma kulinda na kudumisha maadili ya utumishi katika taasisi wanazoziongoza ili kudhibiti mianya ya rushwa pamoja na uvujishwaji wa taarifa za siri za serikali
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Kusirie Swai wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya Maadili kwa viongozi wa umma yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa Umma kwa kushirikiana na chuo cha uhasibu Arusha yaliyofanyika Jijini Mwanza ambapo amesema maadili ni nguzo muhimu katika kuendeleza Taifa lolote kwani yanasaidia kujenga imani kwa wananchi juu ya watumishi wanaowawakilisha kwenye utumishi wa umma.

“Maadili yanasaidia kujenga tija na thamani ya rasilimali jinsi zinavyotumika kwa masilahi ya Taifa lao kama madini na maji kwa manufaa ya wote.” Ndugu Swai.
Katika hatua nyingine Swai ameongeza kuwa sehemu yoyote ambayo ina maadili huzalisha watu wawajibikaji na wenye uwazi hivyo amewaomba wananchi pamoja na viongozi kuzingatia hilo ili kuepukana na suala la mmomonyoko wa maadili.

Kwa upande wake Katibu msaidizi kutoka Ofisi ya Rais sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa, Godson Kweka amebainisha kuwa mafunzo hayo ni programu maalum kwa viongozi wote wa umma ikiwa ni kwa ajili ya kuwakumbusha wajibu wao.
“Mafunzo haya yatasaidia kukuza na kuendeleza maadili ya viongozi umma na yatasaidia kubadilishana uzoefu katika kuhakikisha sheria na miongozo ya maadili inafuatwa.” Amebainisha Kamishna Kweka.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ambao pia ni viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma mkoani Mwanza pamoja na mambo mengine wameiomba Serikali kuchukua hatua za kinidhamu kwa baadhi ya watumishi wanaokiuka sheria za maadili ya Utumishi wa Umma.