Na Saulo Stephen – Singida.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amezitaka taasisi za Serikali kuhakikisha zinalipa madeni ya pango na ardhi kabla ya kuhitimishwa kwa mwaka wa bajeti, ili kuiwezesha Serikali kutekeleza kwa ufanisi shughuli zake za maendeleo.
Dkt. Mganga ametoa kauli hiyo katika kikao kazi kilicholenga kujadili hali ya madeni hayo, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Singida.

Amesema kuwa kwa sasa taasisi za Serikali zinadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 2.1, fedha ambazo zingesaidia kwa kiasi kikubwa kugharamia miradi ya maendeleo huku akiongeza kuwa ni muhimu kwa taasisi hizo kutimiza wajibu wao wa kifedha kwa wakati, ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Awali, akimkaribisha Katibu Tawala wa Mkoa, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza, amesema kuwa hadi sasa ofisi ya ardhi imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 1.3, huku lengo la Serikali likiwa ni kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 3.6.

Aidha amezihimiza taasisi zinazodaiwa kufika katika Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa ili kujadiliana na kupanga utaratibu bora wa kukamilisha malipo hayo kwa wakati.