Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kupitia taarifa yake kwa umma limeeleza kuwa taarifa
inayosambaa mitandaoni ikidai kuwa uchunguzi wa saratani ya matiti kwa kutumia biopsia husababisha saratani kuenea si ya kweli na haina msingi wa kisayansi.
Taarifa hiyo, iliyotolewa Machi 2, 2026 na Msajili Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala, Lucy Mziray imeeleza kuwa Biopsia ni njia salama, ya msingi na inayotambulika duniani kote katika kuthibitisha aina ya saratani, ili kusaidia kupanga matibabu sahihi kwa wakati.
“Madai kwamba biopsia husababisha saratani kusambaa ni upotoshaji unaoweza kuhatarisha maisha ya wagonjwa. Aidha, Baraza linapenda kufafanua kwamba mtu anayeonekana kwenye video inayosambazwa si mtaalamu wa Tiba Asili na wala hatambuliwi na baraza lolote la kitaaluma nchini,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, baada ya ufuatiliaji Baraza hilo limedai kugundua muhusika anajihusisha na biashara
za bidhaa za kimtandao “network marketing” na wala hatakiwi kuelimisha jamii masuala ya afya, huku likielekeza kuwa Wanataaluma wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, Wafanyabiashara na wajasiriamali wote wa bidhaa mbalimbali wanaotoa elimu au kutumia bidhaa hizo kwa madai ya kimatibabu waondoe mara moja
matangazo yote yanayopotosha jamii.
“Yanaweza kuchelewesha wagonjwa
kupata matibabu sahihi na kuwanyima haki yao ya msingi ya huduma bora za afya.
Wananchi wanahimizwa kutotegemea taarifa zisizothibitishwa, na badala yake kufika
katika vituo rasmi vya afya vinavyotambulika kwa ajili ya uchunguzi na matibabu sahihi
yanayotolewa na wataalamu waliothibitishwa,” ilizidi kufafania taarifa hiyo.
